Wachezaji Yanga watoa ahadi nzito

By Adam Fungamwango , Nipashe
Published at 08:18 AM Jan 15 2025
NAHODHA Msaidizi wa Yanga, Dickson Job.
Picha:Mtandao
NAHODHA Msaidizi wa Yanga, Dickson Job.

NAHODHA Msaidizi wa Yanga, Dickson Job, amebainisha kuwa yeye na wachezaji wenzake wamejipanga kucheza mchezo wa mwisho dhidi ya MC Alger ya Algeria kama hawatokuwa na mechi nyingine yoyote chini ya ardhi.

Yanga inatarajia kucheza mchezo wa mwisho wa Ligi ya Mabingwa Afrika hatua ya makundi, dhidi ya MC Alger, Jumamosi ijayo kwenye Uwanja wa Benjamin Mpaka, Dar es Salaam.

Ni ushindi tu ndiyo utawafanya Mabingwa hao wa Tanzania Bara kufuzu hatua ya robo fainali kutoka Kundi A.

"Nimekaa na wachezaji wenzangu, tumeahidiana kuwa Jumamosi ndiyo siku ya kumaliza kazi, ndiyo fainali yetu, tumeapizana kwenda kucheza kama vile hatutokuwa na mchezo mwingine tena chini ya ardhi baada ya hapo. Yaani baada ya hapo hatutocheza tena. Maana yangu ni kwamba wachezaji tunatakiwa kujitoa bila kubakisha akiba ya chochote kile wala kujali lolote, nguvu, majeraha, kama hatutakuwa na mechi zingine mbele yetu," alisema Job.

Alisema iwapo watashindwa kufanya hivyo, basi hata mchezo wa Jumapili iliyopita ambao walishinda bao 1-0 dhidi ya Al Hilal Omdurman ya Sudan, hautokuwa na maana yoyote.

Yanga ilishinda bao 1-0 ikiwa ugenini, Uwanja wa De la Capitale, jijini Nouakchott, nchini Mauritania, ambako timu hiyo inautumia kama uwanja wake wa nyumbani, kutokana na machafuko ya kisiasa kwao Sudan.

"Tulikuwa kwenye nafasi mbaya, tulizihitaji sana pointi hizi ili kuweza kujitengenezea mazingira mazuri ya kwenda robo fainali, sasa kama tumeshinda mchezo huu, haitokuwa na faida yoyote endapo hatutoshinda mchezo wa mwisho nyumbani, tulitaka kushinda huu ili tukamalizie mchezo kwa ushindi kwetu, hivyo baada ya hapa, tunageukia mchezo unaofuata ambao ni wa kufa ama kupona," alisema beki huyo anayemudu kucheza kati na pembeni kulia, ambaye alizungumza akiwa nchini humo.

Ofisa Habari wa Klabu hiyo, Ali Kamwe, alisema pamoja na ushindi huo hawawezi kuendelea kufurahia, badala yake kazi inahamia Dar es Salaam.

"Tuna mechi ya mwisho nyumbani, ni mechi muhimu sana kwa Yanga, tulikuwa na mechi ngumu, jasho limetuvuja kweli kweli, tumebakisha dakika 90 za moto ambazo zitamaliza mchezo wa Kundi A, na sisi tutakwenda robo fainali," alisema Kamwe.

Yanga na MC Alger zote zinawania nafasi moja, baada ya Al Hilal kufuzu ikiwa na pointi 10, ingawa bado haijawa na uhakika wa kumaliza ikiwa kinara wa kundi.

Yanga, iko nafasi ya tatu ya msimamo ikiwa na pointi saba, hivyo inahitaji ushindi pekee ili kufuzu, ambapo itafikisha pointi 10 na kuiacha MC Alger ikisalia na pointi zake nane.

Wakati huo huo, baadhi ya mashabiki wa MC Alger wameanza kutua nchini tayari kwa kuisapoti timu yao kwenye mchezo huo.

Kundi la kwanza la baadhi ya mashabiki wa timu hiyo limetua jana jijini Dar es Salaam, huku kundi lingine likitarajiwa kuwasili na timu.

MC Alger, yenye pointi nane kwenye nafasi ya pili, yenyewe inahitaji sare ya aina yoyote ili kufuzu kwani ikifanikiwa itakuwa imefikisha pointi tisa na Yanga itaambulia pointi nane pekee katika michezo sita ya hatua hiyo ya makundi.