KLABU ya Pamba Jiji iko kwenye hatua za mwisho za kumpeleka straika George Mpole Klabu ya Singida Black Stars kwa mkopo kabla ya kufungwa kwa dirisha dogo la usajili leo saa sita usiku.
Taarifa kutoka ndani ya Klabu ya Pamba Jiji, zimeleza kuwa mbali na Mpole, klabu hiyo pia inatarajiwa kumpekeka straika wao mwingine raia wa Ghana, Erick Okutu kwa mkopo katika Klabu ya KenGold, ingawa mwenyewe anapinga akitaka avunjiwe mkataba kama hawataki kuendelea naye.
Chanzo kutoka ndani ya klabu hiyo kimesema kuwa Pamba, inamuondoa Mpole kutokana na kutoridhishwa na kiwango chake, huku Okutu akitajwa kuwa ni mtovu wa nidhamu.
Aidha, chanzo kingine kimedai kuwa Singida Black Stars, imemuomba Mpole ili kwenda kusaidiana na Elvis Rupia kwenye safu ya ushambuliaji, wakiamini anaweza kufanya vema katika timu yao kuliko huko aliko.
Kinasema Singida Black Stars, imetumia fursa hiyo, baada ya kuwapatia Pamba Jiji, wachezaji Habib Kyombo, Hamad Majimengi na kipa Mohamed Kamara, kipa wa zamani wa Horoya FC, raia wa Sierra Leone.
"Baada ya kukamilisha usajili wa washambuliaji, Habib Kyombo na Mathew Tegisi Momanyi tumeona Mpole tumtoe kwa mkopo na Singida Black Stars imeonesha nia ya kumhitaji, lengo ni kudumisha uhusiano uliopo baina yetu,” kilisema chanzo hicho.
Pamba imemsajili straika Momanyi kutoka Shabana FC ya Kenya, ambapo anatarajiwa kuwa miongoni mwa wachezaji watakaoivaa Dodoma Jiji katika mchezo wao kwa kwanza wa mzunguko wa pili wa Ligi Kuu, itakayoanza kutimua vumbi tena kuanzia Machi Mosi, mwaka huu.
Mpole aliyejiunga na kikosi hicho msimu huu baada ya kuachana na FC Lupopo ya DR Congo, anakumbukwa zaidi msimu wa 2021/22, alipoibuka mfungaji bora wa Ligi Kuu Bara akitupia mabao 17, akimuacha 'solemba', kwa tofauti ya bao moja, straika wa Yanga wakati huo ambaye kwa sasa anaichezea, Pyramids ya Misri, Fiston Mayele.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED