CAF yafungia mashabiki Simba, Fadlu afunguka

By Adam Fungamwango , Nipashe
Published at 08:14 AM Jan 15 2025
CAF yafungia mashabiki Simba.
Picha: Mtandao
CAF yafungia mashabiki Simba.

SHIRIKISHO la Soka Afrika (CAF), limeifungia Klabu ya Simba kuingiza mashabiki kwenye mechi yao ya mwisho ya hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya CS Constantine ya Algeria, unaotarajiwa kuchezwa Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam Jumapili wiki hii.

Kutokana na maamuzi hayo ya CAF, Klabu ya Simba imesitisha mauzo ya tiketi ya mchezo huo.

Taarifa kutoka CAF zilizotoka jana, zizothibitishwa na Klabu ya Simba jioni zinaeleza kuwa adhabu hiyo inatokana na vurugu zilizotokea kwenye mchezo wao dhidi ya CS Sfaxien ya Tunisia uliopigwa Desemba 15, mwaka jana, kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, uliomalizika kwa kupata ushindi wa mabao 2-1.

Taarifa iliyotolewa jana jioni na klabu hiyo ilisema imepokea maamuzi kutoka CAF kuhusu vurugu zilizojitokeza na kuifungia kwa michezo miwili.

"Hata hivyo, pamoja na kufungiwa michezo miwili, adhabu hiyo imepunguzwa na kuwa mchezo mmoja kucheza bila mashabiki pamoja na faini ya Dola za Kimarekani 40,000.

"Tunapenda kuufahamisha umma kuwa tunaendelea kufanya utaratibu ili kushughulikia uamuzi huo," ilisema sehemu ya taarifa hiyo.

Kutokana na adhabu hiyo ya CAF, klabu hiyo imetangaza kusitisha mauzo ya tiketi ya mchezo wa raundi ya sita ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya CS Constantine.

"Kwa mashabiki ambao wameshanunua tiketi ni kwamba zitatumika kwenye mchezo ujao wa robo fainali. Klabu yetu itaendelea kusimamia taratibu, kanuni na sheria zinazozingatia usalama kwa jumla katika michezo," ilisema taarifa hiyo.

Vurugu zilitokea kwenye mchezo huo dakika za mwisho baada ya Kibu Denis kufunga bao la pili, ambapo baadhi ya viongozi, benchi la ufundi na wachezaji wa CS Sfaxien walivamia uwanja kutaka kumpiga mwamuzi kwa madai dakika zilikuwa zimemalizika, lakini jukwaani pia kulikuwa na vurumai kati ya mashabiki wa Simba na CS Sfaxien, ambapo vitu kadhaa viliripotiwa kung'olewa.

Wakati huo huo, Kocha Mkuu wa Simba, Fadlu Davids, amesema tayari wamefahamu mfumo ambao wapinzani wao, CS Constantine, watacheza Jumapili ijayo, nao ni 'kupaki basi' ili kutafuta sare, hivyo kwa siku zilizobaki atazitumia kuwafundisha wachezaji wake jinsi ya kutegua mitego yao.

Fadlu alitoa siri hiyo baada ya kutua nchini alfajiri ya jana wakitoka Angola, ambako timu yake ilifanikiwa kutinga hatua ya robo fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika, ikilazimisha sare ya bao 1-1 dhidi ya Bravos do Maquis, katika mchezo uliochezwa Jumapili iliyopita kwenye Uwanja wa Novembro 11 jijini Luanda.

Alisema anachotaka kukifanya katika mchezo wa Jumapili ni kuutawala mchezo kwa asilimia nyingi, kuvunja mitego yote, kupasua ukuta waliouweka na mwishowe kuibuka na ushindi katika mchezo huo.

"Najua wanahitaji sare ili kuongoza kundi, kwa hiyo watakuja kucheza nyuma ya mpira, katika siku hizo zilizobaki za mazoezi nitakachofanya ni kuwaelekeza wachezaji wangu jinsi gani ya kukabiliana nayo. Haitokuwa CS Constantine kama ile iliyocheza ikiwa kwao nchini Algeria, tunahitaji kuwasukuma kwa nguvu langoni kwao, tunatakiwa kuwa na ubunifu, kushambulia bila kuchoka kwa ajili ya kuvunja mitego yote, kupasua ukuta waliouweka na mwishowe kuibuka na ushindi," alisema Fadlu.

Alirejea tena kauli yake kuwa ushindi katika mchezo wa Jumapili ijayo ni muhimu mno licha ya kwamba wameshatinga hatua ya robo fainali, kwani unaweza kuwa njia ya kuwarahisishia kazi kwenda kwenye hatua ambayo wanachama na mashabiki wa Simba wanaihitaji sana, nusu fainali. 

"Mpango wa kwanza wa robo fainali umekamilika, wa pili ni kuongoza kundi ili tupate nafasi ya kuanzia ugenini pindi droo itakapopangwa na kumalizia nyumbani, itatusaidia sana kwenye malengo yetu kwani tukiwa tunahitaji ushindi mechi ya mwisho nyumbani, hatuwezi kushindwa," alisema Fadlu.

Katika mchezo huo, CS Constantine itaingia ikiwa inahitaji sare yoyote ili kuongoza Kundi A, kwani iko kileleni na pointi zake 12.

Simba, iliyo nafasi ya pili na pointi zake 10, inahitaji ushindi ili ifikishe pointi 13 na kuipiku CS Constantine ambayo kama itafungwa itasalia na pointi 12.

Iwapo timu hizo zitatoka sare, Constantine itaongoza kundi ikiwa na pointi 13 na Simba itamaliza ya pili ikiwa na pointi 11.