Abiria 1,000 treni ya SGR wasafiri Dar- Dodoma, wengi wakosa nafasi

By Paul Mabeja ,, Pilly Kigome , Nipashe
Published at 12:39 PM Jul 26 2024
Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Reli Tanzania (TRC), Masanja Kadogosa.

SAFARI ya kwanza ya treni ya kisasa (SGR) kutoka Dar es Salaam hadi Dodoma, ilianza rasmi jana kwa takriban abiria 1,000 huku maelfu ya watu wakijitokeza na wengi kukosa nafasi baada ya mabehewa yaliyoandaliwa kujaa.

Safari hiyo ilianza katika kituo kikuu cha Dar es Salaam saa 11:19 alfajiri huku Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Reli Tanzania (TRC), Masanja Kadogosa, akiwaambia waandishi wa habari kwamba mabehewa 14 yaliandaliwa lakini kutokana na mwitikio wa abiria kuwa mkubwa, wengi walikosa nafasi.  

“Kwa jumla walijitokeza abiria wengi jambo ambalo hatukulitarajia kwamba kungekuwa na mwitikio kama huu. Hakuna hata siti (kiti) iliyosalia katika mabehewa ya madaraja yote. Hata tungefunga mabehewa 20 kwa ajili ya safari hii ya kwanza kutoka Dar es Salaam hadi Dodoma, ni dhahiri kwamba yangejaa kutokana na hamu ya Watanzania wengi kutumia usafiri huu ambao kwa kweli unaokoa muda,” alisema Kadogosa.

 “Tunamshukuru Mungu safari ya kwanza tumeianza leo Julai 25 kama ilivyokuwa imepangwa. Tumesafiri na baadhi ya viongozi wakiwamo wakurugenzi, wabunge na baadhi ya wajumbe wa bodi kwa kutumia usafiri huu,” aliongeza. 

Pamoja na kuanza kwa safari hiyo, alisema wanamshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa juhudi zake kubwa kwa kuwauliza kila hatua pamoja na changamoto walizokuwa wanakabiliana nazo katika kuanza safari hiyo. Alisema Rais pia alikuwa anawauliza mara kwa mara nini wanahitaji ili mradi safari hiyo ianze.

Licha ya kuanza kwa safari hiyo, Kadogosa alisema usafiri huo utazinduliwa rasmi na Rais Samia ndani ya wiki mbili  kuanzia sasa.

Akizungumza baada ya kufika Dodoma baada ya kuwasili kwa treni hiyo saa 4:00 asubuhi, Kadogosa alisema treni hiyo ingefika mapema zaidi lakini walisimama kwa muda njiani kwa ajili ya kupisha treni iliyotoka Dodoma.

“Lakini kadiri siku zinavyokwenda tutaendelea kuboresha changamoto ambazo zimejitokeza leo (jana) kama ilivyokuwa wakati tulipoanza safari za Dar es Salaam hadi Morogoro,” alisema.

Kuhusu mwitikio wa abiria kutumia usafiri huo, Kadogosa alisema ni mkubwa hali ambayo inawapa kazi ya kufanya ili kukidhi mahitaji.

"Leo treni ya asubuhi tayari imejaa ya jioni na ya kesho pia imejaa, hivyo tutaendelea kuangalia mwenendo utakavyokuwa ili kuongeza safari kama ilivyokuwa katika safari za Dar- Morogoro" alisema.

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Ardhini (LATRA), Habibu Suluo, aliishukuru serikali kwa kufanikisha safari ya kwanza ya treni ya SGR kutoka Dar es Saalam kuja Dodoma. 

“Maono ya Rais wetu yametimia leo (jana). Tumepokea  kwa mara ya kwanza treni ya umeme kutoka Dar es Saalam. Nitumie  fursa hii niwaombe Watanzania tutunze miundombinu hii ambayo serikali imewekeza kiasi kikubwa cha fedha kufanikisha mradi huu wa kimkakati,” alisema. 

KAULI YA ABIRIA 

Baadhi ya abiria, akiwamo  Rose Mchau, mkazi wa Dar es Salaam, walionyesha furaha kwa kutumia aina hiyo ya usafiri ambayo inatumia muda mfupi kulinganisha na aina zingine za usafiri wa nchi kavu.  

“Kwanza nimevutiwa sana na kutumia saa chache ya kusafiri. Pili, nimependa mazingira ni masafi sana kama tuko airport (uwanja wa ndege), hivyo nitawahimiza watu wa Dodoma ambako kwa sasa nafanya kazi, waje kwa wingi kutumia usafiri huu kwa kuwa si uzushi kama tulivyojua awali,” alisema. 

Mohamed Makongoro, mkazi wa Tabata ambaye amepata tenda ya shughuli zake za uchukuaji picha, alisema ameona atumie usafiri huo ili kuendana na muda kuliko kutumia usafiri wa basi. 

“Tumpe hongera sana Mama (Rais) kutukamilishia usafiri huu. Nimefurahi  sana  kwani usafiri huu umekuja kuimarisha uchumi kwa sisi watu wenye uchumi wa chini na kati tutafanya biashara na mambo yetu kwa wakati” alisema 

Amina Hassan alisema usafiri huo wa treni ya kisasa utakuwa mkombozi kwa makundi yote kutokana na kuokoa muda wa safari tofauti na ilivyokuwa kwa usafiri mwingine.

·    Imeandikwa na Pilly Kigome (DAR) na Paul Mabeja, DODOMA.