Mwenge kuzindua miradi ya thamani ya Bil. 24. 9 Mara

By Sabato Kasika , Nipashe
Published at 08:55 PM Jul 25 2024
Kanali Evans Mtambi akizungumzia ujio wa Mwenge wa Uhuru mkoani humo.
Picha: Mpigapicha Wetu
Kanali Evans Mtambi akizungumzia ujio wa Mwenge wa Uhuru mkoani humo.

MIRADI 72 ya maendeleo yenye thamani ya Sh. bilioni 24. 9, inatarajiwa kuzinduliwa na mbio za Mwenge Uhuru, mkoani Mara, zitakazoanza kesho na kukimbizwa kwa muda wa siku tisa.

Hayo ni kwa mujibu wa Mkuu wa Mkoa huo, Kanali Evance Mtambi wakati akizungumza na waandishi wa habari mjini Musoma leo na kufafanua kuwa utakimbizwa katika wilaya zote sita za mkoa huo.

"Baadhi ya miradi ni ya sekta ya elimu, kilimo, ujenzi, maji, afya, mifugo, mazingira, ustawi wa jamii, viwanda na biashara inayotekezwa  kwa fedha vya vyanzo mbalimbali vya mapato," amesema Mtambi.

Kanali Mtambi ametaja michango hiyo ni ya wananchi Sh. bilioni 2.4, mapato ya halmashauri Sh. bilioni 1.6, serikali kuu Sh. bilioni 12.8 na fedha za wahisani Sh. bilioni 7.9.

"Niwashukuru wananchi wa Mkoa wa Mara waliochangia kwa hali na mali katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo, na ninawaomba waendelee na utaratibu huo wa kushirikiana na serikali katika kuleta maendeleo," amesema.

Mkuu huyo wa mkoa amesema, maandalizi ya kupokea mwenge  mkoani humo, yamekamilika na kwamba wapo tayari kuukimbiza katika maeneo mbalimbali, kwa ajili ya kuzindua miradi ya maendeleo.

Aidha, amewaalika wananchi wote kwenye maadhimisho ya miaka 60 ya Mwenge wa Mwitongo, yatakayofanyika Agosti mosi mwaka huu, nyumbani kwa Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere, Mwitongo, Butiama.

"Niwaombe wananchi wote kwa umoja wetu tuupokee Mwenge wa Uhuru na tuhakikishe unamaliza salama mbio zake katika mkoa wetu uendelee na mbio zake mikoa mingine ili nasi twende kwenye maadhimisho ya miaka 60 ya Mwenge wa Mwitongo,"amesema.