Makandarasi wafundwa usimamizi mikataba katika miradi ya ujenzi

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 06:46 PM Jul 26 2024
Mhandisi David Jere, Mratibu wa mafunzo, Mkuu wa Idara ya Utafiti na Maendeleo.

Makandarasi wameaswa kuzisimamia kampuni zao vizuri na kuzingatia misingi ya Usimamizi wa Mikataba katika utekelezaji wake. Aidha, wameaswa kutumia wataalamu wa fani stahiki katika makampuni yao na katika utekelezaji wa miradi ili kuepuka changamoto zinazoweza kuathiri utendaji wa makampuni yao au utekelezaji wa miradi.

Akizungumza katika mafunzo hayo yaliyofanyika kwa siku tatu mkoani Dodoma, Mratibu wa mafunzo, Mkuu wa Idara ya Utafiti na Maendeleo kwa Makandarasi, Mhandisi. David Jere, alisema kuwa lengo ni kuwajengea uwezo na kukuza ujuzi kwa makandarasi pamoja na waajiri kuhusiana na namna nzuri ya kusimamia mikataba ya kazi za ujenzi.

“Kupitia mafunzo haya wamejifunza mada mbalimbali kutoka kwa mwezeshaji ikiwemo mambo ya kuzingatia katika viwango vya kazi, thamani ya kazi, gharama ya kazi na muda wa utekelezaji wa kazi za ujenzi”, alisema Mhandisi. Jere.

Sambamba na hayo alisisitiza kuwa makandarasi washiriki mafunzo mbalimbali yanayoandaliwa na CRB ili kuwaongezea thamani kwasababu ujuzi huwa unaongeza ufanisi katika shughuli yoyote ile na wafanye kwa vitendo yale yote waliyofundishwa, kushirikiana   na kutimiza wajibu wao katika miradi mbali mbali na kuwa wafanyabiashara wa kweli na halali bila kukwepa kulipa kodi, kughushi nyaraka na kufanya kazi kwa weledi na kwa kuzingatia sheria za nchi.

Mhandisi Mshauri, Alex Kijugo kutokea RUWASA alisema amefurahishwa na mafunzo hayo kwani yamemuwezesha kujua majukumu yake ipasavyo kwa kutofautisha baina ya majukumu ya Mkandarasi na Mshauri.

Hata hivyo Kijugo alisema muda, ubora wa kazi na gharama zake ni mambo ya muhimu aliyoyachukua zaidi katika kuhakikisha anakwenda kusimamia ipasavyo katika suala zima la usimamizi wa Mikataba.

"Makandarasi wengi wamekuwa wananyimwa haki zao ila kwa waliohudhuria mafunzo haya, ninaamini watakwenda kuzijua haki zao katika kusimamia Mikataba yao mbalimbali ya kazi wanazozipata”, alisema Kijugo.

Kwa upande wake Gunilla Nyagawa, Meneja wa Shughuli kutokea Africentric Company Ltd aliishukuru Bodi kwa kuwezesha utolewaji wa kozi maalumu ya Mafunzo ya Usimamizi wa Mikataba kwa Makandarasi, nakusema kuwa imempa mwanga mzuri wa namna sahihi na bora wakati wa kutekeleza majukumu yake ya ukandarasi.

"Tumejifunza mambo mapya, tumejifunza mambo mazuri sana lakini jambo la msingi ambalo nimelipenda zaidi katika usimamizi mzuri wa Mikataba ni suala la kuzingatia muda, kwani Mkandarasi mzuri ni yule mwenye kujali muda wa kutekeleza kazi aliyopatiwa hali itakayomjengea uaminifu kutoka kwa wengine" alisema Nyagawa.

Aidha, Nyagawa alisema jambo lingine ambalo limekuwa ni msaada kupitia mafunzo hayo ni hali ya kupata majibu ya mambo ambayo yamekuwa na changamoto wakati wa kutekeleza majukumu yao na hivyo kupitia wataalamu husika ambao ni wawezeshaji wamekuwa ni msaada mkubwa kwao.

Mwisho Nyagawa alitoa rai kwa Makandarasi kuzichangamkia fursa mbalimbali za mafunzo yanayokuwa yakiandaliwa na Bodi ya Usajili wa Makandarasi (CRB) ili kujengewa uwezo mzuri utakaowasaidia wakati wabutendaji kazi wao.

Mafunzo haya yamewakutanisha washiriki zaidi ya 90 kutoka mikoa 13 hapa nchini wakiwemo Makandarasi na Waajiri.