Uswisi yaipongeza Tanzania kuelekea uchaguzi

By Sabato Kasika , Nipashe
Published at 06:36 PM Jul 26 2024
Balozi wa Uswisi nchini anayemaliza muda wake, Didier Chassot
Picha: Sabato Kasika
Balozi wa Uswisi nchini anayemaliza muda wake, Didier Chassot

USWISI imeipongeza Tanzania kwa namna inavyochukua hatua mbalimbali katika kuleta mbadiliko ya kisiasa, kijamii na kiuchumi, wakati huu inapoelekea katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa na Uchaguzi Mkuu.

Pongezi hizo zimetolewa jana na Balozi wa Uswisi nchini anayemaliza muda wake, Didier Chassot, wakati wa maadhimisho ya Siku ya Kitaifa ya Uswisi, yaliyofanyika katika makazi ya balozi, jijini Dar es Salaam.

“Jambo la muhimu ni kuwa na mfumo wa utawala bora (wa kidemokrasia) unaoweza kutoa haki usawa, uhuru wa kujieleza, maendeleo, ustawi, amani na usalama, hicho ndicho ambacho tunakiona kwa serikali ya Tanzania,” alisema.

Balozi Chassot alisema Tanzania inaendelea kuimarisha mfumo wa kidemokrasia, unaolenga kuwa na uchaguzi za uwazi, unaoaminika kwa wengi.

Alisema mfumo huo unaleta haki kwa wote hata katika huduma kwa jamii kutoka katika mamlaka mbalimbali.

Alisema Tanzania inaendelea kuchukua hatua mbalimbali za kutatua changamoto kwa lengo la kutaka kila Mtanzania anakuwa na maisha bora.

Baadhi waliohudhuria maadhimisho hayo.
Balozi huyo alihimiza umuhimu wa kuzingatia Mkataba wa Geneva ili kulinda raia wasio na hatia ambao wamekuwa wakiteseka kwa kujeruhiwa au kupoteza maisha katika vita inayoendelea katika nchi mbalimbali.

 “Mataifa yote ambayo ni wanachama wa mkataba huo yanapaswa kuhakikisha yanazingatia utashi wa kisiasa kwa kuheshimu mkataba huo, ili kuendelea kuokoa mamilioni ya maisha yanayotishiwa na migogoro mingi duniani kote,” alisema.

Alisema mkataba huo ukizingatiwa maelfu ya wanafamilia waliotengana kutokana vita wataungana, huku akisisitiza umuhimu wa kuheshimiwa kwa mkataba huo, ambao unalenga kuwalinda watu wasio na hatia wakati wa vita.

Naibu Waziri Wizara ya Nchi, Ofisi ya Rais, Fedha na Mipongo Zanzibar, Juma Makungu Juma, alisema kwa miaka mingi, Uswisi imeendelea kuwa mshirika mkuu wa maendeleo wa Tanzania, kwa kutoa misaada katika sekta mbalimbali zikiwamo elimu ya afya, utalii, biashara na uwekezaji na maendeleo ya jamii.

Juma aliomba serikali ya Uswisi kushirikiana na Tanzania katika eneo la teknolojia ya viwanda vya ndani katika kuongeza thamani wa mazao kama korosho, pamba, chai, kahawa ili Watanzania waendelee kuinuka kiuchumi.

“Lakini pamoja na hayo, ninatoa tena ombi lingine kwamba, serikali ya Uswisi iangalie wa kurejesha upya safari zake za ndege nchini, kwa manufaa ya pande mbili, yaani Uswisi na Tanzania ambazo kwa sasa hazipo,” alisema Juma.