Wananchi sasa ni wakati wa kuhakiki majina waliojiandikisha

Nipashe
Published at 12:37 PM Oct 22 2024
Wapigakura
Picha:Mtandao
Wapigakura

UANDIKISHAJI wa Daftari la Wapigakura la Wakaazi, umekamilika mwishoni mwa wiki, kwa ajili ya kujiandaa na uchaguzi wa Serikali za Mitaa, unaotarajiwa kufanyika Novemba 27, mwaka huu.

Umuhimu wa kujiandikisha kwenye daftari hilo ni kutoa haki kwa wananchi wote wanaostahili kupiga kura kuchagua viongozi wao wa mtaa wanao ona wanaweza kutatua kero zao.

Uchaguzi huu ni muhimu kwa kuwa kero zote za mitaa zinapaswa kushughulikiwa kuanzia ngazi za mitaa kwa sababu viongozi watakaochaguliwa ndio wako karibu na wananchi na ni rahisi kuwafikia kwenye mitaa yao.

Kupitia uandikishaji uliofanyika, jukumu la kila kituo ni kubandika majina yote ya watu waliojiandikisha na kisha wananchi wanapaswa kuyahakiki ili kuona yako sahihi na kama kuna watu ambao wamejiandikisha, lakini hawastahili kwa kukosa sifa, itolewe taarifa ili ifanyiwe kazi kuondoa malalamiko.

Moja ya kigezo cha kukosa sifa ya kujiandikisha kwenye daftari hilo ni kama aliyejiandikisha, hajafikisha umri wa miaka 18 na sio raia wa Tanzania na mkazi wa mtaa husika.

Watu wengi wamekuwa wakijiuliza mbona wakati wa kujiandikisha mtu alikuwa akiulizwa majina yake na mtaa anaoishi tu bila uthibitisho mwingine.

Ufafanuzi uliotolewa ni watu kwenda kwenye vituo na kuhakiki majina yao na wale wanaoonekana kama hawastahili wawekewe pingamizi kwa uthibitisho.

Imeelezwa kuwa kwenye uandikishaji ilihakikishwa kuwa kuna mawakala wa vyama ambao walipewa fursa ya kuhakikisha wanaojiandikisha ni wakazi halali wa mitaa hiyo.

Hivyo, imefafanuliwa kuwa wasiwasi kwamba kunaweza kukatokea udanganyifu wa watu wasiokuwa na sifa ya kujiandikisha wanaweza kujipenyeza uondolewe.

Kwa muda huu ambao majina yatabandikwa vituoni ni vyema wananchi wakatumia fursa hiyo kujitokeza kwenda kuhakiki majina ili kuondoa usumbufu wakati wa kupiga kura unapowadia.

Ni jukumu pia la wahusika kwenye mitaa na viongozi kutoa ushirikiano katika hili ili kuondoa malalamiko na sintofahamu wakati wa uchanguzi.

Uchaguzi wa serikali za mitaa ni muhimu sana kwa wananchi kwa sababu kero nyingi huanza kutatuliwa kwenye mitaa na zinaposhindika ndio huenda kwenye ngazi za juu.

Viongozi wanaochaguliwa ni lazima watimize wajibu wao kwa kushirikiana na wananchi wanaowachagua na kusikiliza kero kwa kuzitatua au kutoa taarifa kwa wananchi wao pale kunapojitokeza changamoto ya aina yoyote ile.

Mara nyingi wananchi wamezoea kuona viongozi wanapochaguliwa wanabweteka kwa kutotoa ushirikiano hata wanapofikishiwa kero mbalimbali zikiwamo za miundombinu mibovu ya barabara kwenye mitaa, tatizo la ulinzi na usalama hali inayosababisha wananchi hao kupoteza imani kwao.

Viongozi wengine wanapoona wananchi wanachukua uamuzi wa kutatua kero hizo kwa kuamua kujichangisha na kutengeneza barabara au kuweka ulinzi, wanadhani kuwa wanataka kunyang’anywa nyadhifa zao.

Wengine hata kuitisha mikutano na wananchi wao ili kujua kero zao wanashindwa na badala yake wanasubiri unapokaribia uchaguzi ndio wanaitisha kikao tena ni cha kutoa lawama badala ya kujibu kero wanazopelekewa.

Wananchi wanapokwambia kiongozi kwamba kwenye mtaa wetu kuna kikundi cha vijana wanaofanya uhalifu, fuatilia na chukua hatua tena kwa kuwashirikisha wananchi wako. Ukifanya hivyo hata kazi yako itakuwa rahisi na wananchi watakupenda kwa sababu umeonesha kuwajali, kuwasikiliza na kutatua kero zao.

Miundombinu ya barabara inapoharibika, kiongozi unapaswa kuwashirikisha wananchi wako ili uweze kusaidiwa na kufanya kazi yao iwe rahisi.