Waziri: Polisi hakikisheni usalama Uchaguzi S/Mitaa

By Waandishi Wetu , Nipashe
Published at 12:56 PM Oct 22 2024
WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Rais - Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Mohamed Mchengerwa.
Picha: Mtandao
WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Rais - Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Mohamed Mchengerwa.

WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Rais - Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Mohamed Mchengerwa, amevitaka vyombo vya dola nchini, likiwamo Jeshi la Polisi, kuhakikisha vinaimarisha usalama, ili Uchaguzi wa Serikali za Mitaa uwe wa huru na haki.

Ameelekeza umewekwa utaratibu maalumu wa kuzuia udanganyifu katika uchaguzi, ikiwamo mpigakura mmoja kupiga zaidi ya mara moja katika vituo tofauti, akisisitiza watatumia mifumo ya kiusalama kubaini.

Mchengerwa aliagiza hayo jana jijini Dar es Salaam alipofunga uandikishaji wapigakura katika Daftari la Makazi, zoezi lililoendeshwa kwa siku 10 kufikia juzi.

Alisema kuwa baada ya kumaliza hatua hiyo, kuanzia jana mpaka Oktoba 27 mwaka huu, orodha ya wapigakura itabandikwa katika sehemu za matangazo ya uchaguzi ili kuwawezesha wananchi wahakiki majina yao.

Waziri huyo alisema hatua hiyo itawapa fursa wananchi ama kurekebisha majina yao, kubadili taarifa au kufuta jina iwapo aliyeorodheshwa amefariki dunia huku akiwataka waliojiandikisha kufika kuhakiki.

Pia aliwataka wananchi wenye sifa za kuchaguliwa kuwa viongozi, wajitokeze kuanzia Oktoba 26 mpaka Novemba Mosi kutimiza haki yao ya kikatiba kugombea nafasi za uongozi.

Alipoulizwa kuhusu malalamiko ya vyama vya siasa kwamba baadhi ya wanafunzi kujiandikisha, Mchengerwa alisema tuhuma hizo hazina ukweli kwa kuwa katika shule wapo pia wanafunzi waliozidi umri wa miaka 18 ambao sifa zinawaruhusu.

Alipoulizwa kuhusu malalamiko ya CHADEMA na ACT Wazalendo -- eneo la Mererani Arusha uandikishaji ulifanyika mpaka usiku, waziri huyo alisema, "sina malalamiko hayo na sifahamu chochote, kama tungepata taarifa hiyo tungeifanyia kazi, tunataka uchaguzi huru na wa haki.

Mchengerwa alibainisha kuwa jumla ya wapigakura 31,282,331 wamejiandikisha sawa na asilimia 94.83 ya lengo la kuandikisha watu 32,897,8579. Kati yao, wananume ni 15,236,772 sawa na asilimia 48.71 na wanawake ni 16,045,559 sawa na asilimia 51.29.

MAJINA YACHANWA

Baadhi ya maeneo mkoani Mwanza, ikiwamo mitaa ya Iseni, Hospitali pamoja na Aman, yote ya kata ya Butimba, wilayani Nyamagana, majina yalichanwa asubuhi kabla ya uhakiki kuanza.

Katibu wa CHADEMA, Kata ya Butimba, Athelius Audax, alisema licha ya majina hayo kuchanwa katika maeneo mengine, ukiwamo mtaa wa Kanyerere, wamebaini ongezeko la majina tofauti na yale yaliyoshuhudiwa na mawakala wao juzi jioni.

"Majina ya awali katika mtaa wa Kanyerere yalikuwa ni 1,209 lakini leo (jana) tulipokwenda kuhakiki tumekuta majina zaidi ya 3,000 yaliyobandikwa kwenye ubao. Bado tunafuatilia kujua walioongezwa ili kupeleka malalamiko yetu kupostahili," alidai.

Nipashe ilimtafuta Msimamizi wa Uchaguzi Jimbo la Nyamagana, Mkurugenzi Mtendaji wa Jiji la Mwanza Kiomoni Kibamba ambaye alisema kuchana majina ni kwenda kinyume Sheria ya Uchaguzi Na. 48, hivyo hatua kali za kisheria zitachukuliwa kwa yeyote atakayebainika kuhusika kuharibu nyaraka hizo za umma.

"Kuhusu kurejesha  majina hayo yaliyochanwa ili watu wahakiki, yatarejeshwa tena siku ya kupiga kura, tutabandika nakala nyingine vituoni," alisema Kibamba.

*Imeandikwa na Halfani Chusi (DAR) na Vitus Audax (MWANZA)