KITUO cha Ubia wa Sekta ya Umma na Binafsi (PPPC), kimesema kinafanya mazungumzo na Kampuni ya China Overseas Engineering Group Co.Ltd (COVEC), ambayo imeonyesha nia ya kuwekeza Dola za Marekani bilioni moja (Sh.trilioni 2.7) kwa ajili ya ujenzi wa barabara 10 za mzunguko Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa taarifa kwa umma iliyotolewa hivi karibuni na Mkurugenzi Mtendaji wa PPPC, David Kafulila barabara hizo zitaokoa zaidi ya asilimia 20 za fedha zinazopotea kutokana na foleni.
Amesema COVEC wanatekeleza mradi huo wa kimkakati kwa njia ya ubia kati ya sekta binafsi na serikali na kwamba kwasasa wako kwenye hatua mbalimbali za mazungumzo.
"Tayari mwekezaji amefanya kazi za awali kama vile upembezi yakinifu na uchambuzi wa kiuchumi.Kampuni hii inataka kujenga barabara 10 za mzunguko kati yake sota ni za ndani na nne za nje,"amesema.
Kwa mujibu wa Kafulila, utafiti uliofanywa na Shirikisho la wenye Viwanda Tanzania (CTI) mwaka 2020 umebaini kuwa foleni inasababisha biashara kupoteza asilimia 20 za faida zao kutokana na foleni za magari.
Amesema Dar es Salaam ni moja ya majiji yanayokuwa mwa kasi zaidi barani Afrika,hivyo kuna foleni nyakati za asubuhi na jioni watu wakitoka na kurejea nyumbani.
Aidha,Kafulila amesema Kampuni ya COVEC inayomilikiwa na Serikali ya China ina uzoefu wa kutekeleza miradi ya miundombinu mikubwa na ya kati katika takribani nchi 100 duniani yenye thamani ya Dola za Marekani bilioni 12.22.
Pia miradi mingine inayotekelezwa na kampuni hiyo ni maji,umeme,ujenzi wa barabara,nyumba na madaraja.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED