TCRA: Watumiaji simu za 'vitochi' wafikia milioni 56

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 02:47 PM Oct 22 2024
Simu rununu.
Picha:Mtandao
Simu rununu.

RIPOTI ya Takwimu za Mawasiliano Tanzania iliyotolewa na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), imeonyesha kuwa matumizi ya simu za rununu maarufu kama vitochi imeongezeka kutoka asilimia 82.6 hadi 84.83.

Aidha, watumiaji wa simu rununu ni watu mil 56.2 kutoka mil 52 Juni 2024,huku simu janja zikiwa ni mil 22.02.

Ripoti hiyo imeonyesha kuwa hadi Septemba 2024 asilimia ya simu janja kwa idadi ya watu imeongezeka hadi asilimia 33.85 kutoka asilimia 31.55 iliyorekodiwa Juni 2024.

Aidha,ripoti hiyo imeonesha kuwa Mkoa wa Dar es Salaam unaongoza kwa kuwa na laini za simu zaidi ya milioni 14.8,ikifuatiwa na Mwanza yenye milioni 5.3 na Arusha milioni 4.8.

Huku mikoa mitatu yenye laini chache kwa Tanzania Bara na idadi yake kwenye mabano ni Katavi (833,849, Rukwa (1,324,883), na Lindi (1,401,899).

Kwa Tanzania Visiwani mkoa ulioongoza ni Mjini Magharibi laini 510,853,ukifuatiwa na Kaskazini Pemba 124,684,Kusini Pemba 124,684,Kusini Unguja 110,970,na Kaskazini Unguja 73,743.

Aidha,kwa upande wa idadi ya minara ya mawasiliano ya simu Mkoa wa Dar es Salaam 1,156, Mwanza 423, Morogoro 421 na Arusha 409.

Mikoa yenye minara michache ni Katavi 94, Songwe 108, huku Rukwa ambayo ina laini chache ikiwa na minara 205 na Lindi 223.