ILO: Uhamiaji wa kikazi Afrika Mashariki, pembe ya Afrika bado ni tatizo

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 01:39 PM Oct 22 2024
Meneja Programu, Uhamiaji wa kikazi na miradi wa ILO, Aida Awel
Picha: Mpigapicha Wetu
Meneja Programu, Uhamiaji wa kikazi na miradi wa ILO, Aida Awel

ZAIDI ya watu milioni 7.7 kati ya watu milioni 357 kutoka nchi za Afrika Mashariki na pembe ya Afrika ni wahamiaji wa kikazi.

Hayo yalielezwa jana jijini Dar es Salaam katika mkutano wa kimataifa uliohusu mafunzo ya utatuzi wa masuala ya uhamiaji wa kikazi kwa nchi za Afrika uliondaliwa na Shirika la Umoja wa Mataifa linalosimamia masuala ya kazi (ILO).

Akizungumza katika mkutano huo ambao pia uliwajumuisha wataalamu wa takwimu, vyama vya waajili, Meneja Programu, Uhamiaji wa kikazi na miradi wa ILO, Aida Awel alisema tatizo la uhamiaji wa kikazi kwa nchi za Afrika na pembe ya Afrika ni tatizo kubwa.

Alisema idadi ya watu Afrika Mashariki na pembe ya Afrika inafikia milioni 357 lakini kati ya idadi hiyo milioni 7.7 ni wahamiaji wa kikazi.

Alisema wengi ni wahamiaji ambao wamekimbia nchi zao na kufuata ajira nzuri, wengine wamekimbia vita pamoja na  mabadailiko tabia nchi.

Alisema serikali za nchi husika zinapaswa kuweka sera na sheria madhubuti katika kuwalinda watu wake dhidi ya ajira.

Mkurugenzi wa Sensa ya Watu na Takwimu za Jamii kutoka Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), Ruth Minja alisema uhamiaji wa kikazi una visababishi vingi ikiwemo kiusalama, kutokuwepo kwa ajira za kutosha.

Alisema serikali imejipanga katika kudhibiti hali hiyo, kwamba kutatungwa sera kuhakikisha wahamiaji wanaishi katika mazingira salama.