Mpole afungua akaunti ya mabao

By Adam Fungamwango , Nipashe
Published at 12:33 PM Oct 22 2024
George Mpole
Picha:Mtandao
George Mpole

MSHINDI wa Kiatu cha Dhahabu Tanzania Bara msimu wa 2021/22, George Mpole, amefungua akaunti yake ya mabao msimu huu, akifunga bao la kwanza akiwa na timu yake ya Pamba Jiji FC ambayo imeendelea kusotea ushindi wa kwanza wa Ligi Kuu hadi kufikia mchezo wa nane.

Mpole, aliyefunga mabao 17 msimu wa 2021/22, akimzidi bao moja aliyekuwa mshambuliaji wa Yanga, Fiston Mayele, na baada ya hapo akatimkia St Eloi Lupopo ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo, juzi alifunga bao la kusawazisha dakika ya 75, Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza, akiinusuru timu yake kwa kipigo kutoka kwa Kagera Sugar.

Kabla ya kufunga bao hilo, Peter Lwasa alikuwa ameifungia bao Kagera Sugar dakika ya 44, na dakika 90 zikaisha timu hizo zikiwa sare ya bao 1-1.

Sare hiyo, inaendelea kuifanya Pamba Jiji kuwa timu pekee ya Ligi Kuu ambayo haijashinda mchezo wowote msimu huu, ikiwa imefikisha michezo minane.

Timu hiyo ambayo imecheza michezo minane, imetoka sare tano na kupoteza michezo mitatu ikiwa nafasi ya 15, ikikusanya pointi tano tu mpaka sasa.

Pamba Jiji ni miongoni kwa timu tano ambazo zimefukuza makocha wao mpaka sasa, baada ya kumfuta kazi Goran Copunovic, na hivi karibuni imemtangaza kocha Fred Felix Minziro ambaye ni mchezo wake wa kwanza baada ya kuwa kocha akianza na sare.

Wakati huo huo, Klabu ya Kagera Sugar imemtangaza kocha Melis Medo kuwa Kocha Mkuu, akiisimamia timu hiyo kwa mara ya kwanza, akitokea Mtibwa Sugar.

Hivi majuzi alitangazwa kuwa kocha bora wa Septemba, akiwa na kikosi hicho kinachopambana kwenye Ligi ya Championship ili kurejea Ligi Kuu Tanzania Bara msimu ujao.