Polisi yafunguka kisa na mkasa kuwashikilia makada CHADEMA

By Waandishi Wetu , Nipashe
Published at 12:48 PM Oct 22 2024
Msemaji wa Jeshi la Polisi, DCP David Masime.
Picha: Mtandao
Msemaji wa Jeshi la Polisi, DCP David Masime.

JESHI la Polisi limeeleza sababu ya kuwashilikia makada wawili wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kuwa ni madai ya kuvamia vituo vya kuandikisha wananchi katika Daftari la Wakazi na kufanya fujo.

Taarifa iliyotolewa juzi na Msemaji wa Jeshi la Polisi, DCP David Masime, ilieleza kuwa Mwenyekiti wa Jimbo la Iringa, Frank Nyalusi alikamatwa Oktoba 20, 2024 huko Iringa baada ya kutembelea vituo vya kuandikisha wananchi katika Daftari la Wakazi na kulazimisha apewe madaftari hayo.

Kupitia taarifa hiyo, DCP Misime alisema kuwa kabla ya kukamatwa, alipigiwa simu na Jeshi la Polisi ili ajisalimishe kituoni, lakini alikaidi ndipo ikawalazimu askari polisi kwenda kumkamata.

Alisema taarifa zilizosambazwa katika mitandao ya kijamii kuwa kiongozi huyo alipigwa na polisi baada ya kukamatwa si za kweli na kuwataka watanzania kuzipuuza.

"Jeshi la Polisi lingependa kusema suala la kupigwa halipo na aliyeandika hivyo ni kutaka kutia chumvi, ili apate wafuasi wa kushabikia uongo wake," alidai DCP Masime.

Alisema jeshi hilo pia lilimkamata Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Mkoa wa Katavi, Rhoda Kunchela na wenzake Oktoba 19 mwaka huu baada ya kupokea taarifa kuwa walimvamia karani wa uandikishaji wapigakura katika kijiji cha Songambele, wilayani Mlele, mkoani Katavi, kumfanyia fujo na kumnyang’anya daftari alilokuwa anaandikisha wapigakura.

DCP Misime alisema kuwa baada ya kupata taarifa hizo, polisi walianza uchunguzi kwa kupata maelezo ya aliyefanyiwa uhalifu huo na mashahidi wengine, kisha waliwafuatilia na kuwakuta wamejifungia katika nyumba na kufanikiwa kuwakamata na kuwafikisha kituoni kwa hatua zingine za kisheria.

Aliwataja wengine waliokamatwa kuwa ni Festo Mgombele, Juma Masoud, Melkio Melkiades, Mwenyekiti wa CHADEMA Jimbo la Katavi, Meshack Konja na Nsajigwa John.

Alisema Jeshi la Polisi linatoa onyo kwa watu ambao wanafika vituo vya uandikishaji wapigakura kwa nia ya kufanya uhalifu kwa kuwa watakamatwa na hatua za kisheria zitafuatwa, ikiwamo kufikishwa mahakamani.

LHRC YALAANI

Kukiwa na angalizo hilo la polisi, Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) kimelaani vikali kutekwa, kudhalilishwa na kupigwa kwa Katibu Mwenezi wa Baraza la Wanawake CHADEMA (BAWACHA) Taifa, Aisha Machano, kikisisitiza kuwa ni kinyume na mikataba ya kimataifa ambayo Tanzania ni mwanachama.

Akizungumza na vyombo vya habari jijini Dar es Salaam jana, Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo hicho, Dk. Anna Henga alisema wanalaani vikali vitendo hivyo ambavyo vinaendelea katika kipindi hiki cha mchakato wa uchaguzi.

Dk. Anna alisema LHRC inavitaka vyombo vya dola kuwasaka watuhumiwa popote walipo, kuwatia mbaroni na kuwafikisha kwenye vyombo vya sheria ili hatua stahiki zichukuliwe.

"Tunataka vyombo vinavyohusika kufuata sheria pindi vinapomkamata mhusika au wahusika wa uhalifu, afikishwe mahakamani ndani ya muda husika uliotolewa kisheria," alisema.

Mkurugenzi huyo alisema kuwa hivi karibuni kumekuwa na matukio yanayojirudia yanayokwenda kinyume cha haki za binadamu katika maeneo tofauti nchini, jambo ambalo alisisitiza hawatalifumbia macho.

Alisema kuwa jana Oktoba 21 ni Siku ya Haki za Binadamu Afrika na inasikitisha kuona Tanzania inaadhimisha siku hiyo kukiwa na matukio mengi ya viashiria vya uvunjifu wa haki za binadamu, yakijumuisha kukamatwa baadhi ya viongozi wa vyama vya siasa.

"Vitendo vya kunyanyasa na kuumiza wanawake, hususani wanaojihusisha na siasa katika kipindi hiki cha uchaguzi, hakikubaliki hata kidogo kwani ni kinyume cha sheria na haki za binadamu," alionya.

*Imeandikwa na Jenifer Gilla na Pilly Kigome