MIKOPO MTANDAONI; Wakopaji wasimulia madhila ya kutisha-2

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 02:04 PM Oct 22 2024
Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania, Emmanuel Tutuba.
Picha: Nipashe Digital
Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania, Emmanuel Tutuba.

Sehemu ya kwanza ya ripoti hii jana iliangazia orodha ya kasoro za utoaji mikopo ya mtandaoni, huku Benki Kuu ya Tanzania (BoT) ikitoa mwongozo kuhusu uendeshaji huo wiki kadhaa baada ya mwandishi wa gazeti hili kutaka kupata ufafanuzi wake.

Vilevile, Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) ukaweka bayana hauwatambui wakopeshaji hao. Endelea na sehemu ya pili yenye undani wa madhila yaliyomo katika makubaliano ya mikopo hiyo...

---

MMOJA wa waathirika wa mikopo hiyo, Jackline Meena, anasema alikopa Sh. 50,000 lakini alilipa Sh. 250,000 na waliendelea kumdai na alipogoma kulipa waliunda kundi la WhatsApp kisha wakaweka picha yake na kuwaunga watu wote waliohifadhiwa katika simu yake, wakimdhalilisha kuwa amewatapeli fedha.

 "Niliripoti polisi na nilitumia mbinu zangu kuwapeleka polisi hadi kwenye ofisi waliyokuwapo ambayo haikuwa inajihusisha na masuala ya mikopo. Polisi walikamata wafanyakazi wote hadi meneja rasilimali watu ambao walibaini kuwa watu hao ni wa Mkopo Fasta, App inayomilikiwa na raia wa China.

 "Watu wamefukuzwa kazi, watu wameharibiwa ndoa zao kisa mikopo. Unachukua mkopo kwa njia ya mtandao labla Sh. 500,000 ndani ya siku saba. 

"Siku mbili kabla ya kulipa wameshaanza kukutumia matusi. Wanaunda kundi la WhatsApp, wanaweka picha yako kisha wanaanza kuandika matusi," anasema askari polisi aliyeomba hifadhi ya jina lake. Ni miongoni mwa walioshiriki kumkamata Meneja Rasilimali Watu wa App ya Mkopo Fasta.
 Askari polisi huyo anaendelea kueleza kuwa: "Kuna mama mmoja walimsambaza mtandaoni wakiandika: "Mimi Julian, ninauza..." halafu wakaunga namba za simu za watu walio katika simu yake. 

"Wanaingia kwenye mawasiliano ya simu ya mkopaji kisha wanatumia taarifa zake kumdhalilisha. Tumekagua hadi BRELA hawatambuliki, ni kampuni za ujanjaujanja zinazoibia wananchi."

1

Askari polisi huyo anasema ufuatiliaji wao ulibaini walikuwa na ofisi Mwenge, wilayani Kinondoni, lakini baadaye walihamia Mikocheni (Kinondoni).

"Baadhi ya walioshtaki polisi, walirejeshewa fedha zao na fidia ya usumbufu kisha wakaamua kuachana na kesi," anasema askari huyo.

Mbunge wa Viti Maalumu (CHADEMA), Felista Njau, anasema amefanya utafiti tangu mwaka 2020 na kukutana na kero hizo katika majimbo mbalimbali, wakopeshaji hao wanabadili majina ya taasisi zao kila mara, lakini lengo ni kutoa mikopo yenye riba kubwa. Walengwa wakuu ni wanawake.

 "Wanawakopesha wanawake zaidi kwa kuwavutia kwa kuwaambia ni mikopo inatolewa ndani ya muda mfupi na watarejesha kwa urahisi.

"Wanawadanganya riba ni nafuu, wanawake wengi hawajui asilimia 10 ya Sh. 200,000 ni Sh. 20,000, hawawaambii ukweli, nimekuta kuna mikopo yenye riba kubwa mno.
 
 "Kuna mama anakopa Sh. 50,000 lakini anarejesha hadi inafika Sh. 175,000, wanawadanganya kwa dhamana ndogo, wanawake wanadhalilishwa na kufilisiwa na wengine wameachika na kukimbilia mjini kwenda mafichoni baada ya mali zao kama friji, brenda na samani za nyumba kuchukuliwa," anasema mbunge huyo.
 
 Mbunge Felista anasema kuwa katika utafiti wake, amebaini wanawake 65 wamefariki dunia kwa kujinyonga au kunywa sumu katika mikoa minane nchini, huku wengine wakijidhuru na kuachika kutokana na madeni yasiyokwisha.

2

"Tumezalisha ombaomba, dadapoa (wanawake wanaofanya biashara ya ngono), wanajiuza ili wapate kuishi baada ya mtaji wao kudhulumiwa na wakopeshaji ambao wemeingia mtandaoni kwa ajili ya kuibia watu.

"Hali ni mbaya. Hiyo mikopo ya mitandaoni, wanaambiwa andika majina ya watu wawili unaowajua, akishatumiwa Sh. 50,000 ya mkopo baada ya siku mbili wale alioweka namba zao wanaanza kudaiwa. Akichelewa kulipa, picha inawekwa mtandaoni 'huyu ni mdaiwa sugu, ni malaya anajiuza' na udhalilishaji mwingine," Felista anasema.

 Mbunge huyo anaitaka BoT kuzifuatilia kwa karibu taasisi ndogo za fedha (microfinance) na kuchukua hatua kali kwa kuwa sheria zipo na hatua zinapaswa kuchukuliwa dhidi ya udhalilishaji unaoendelea hivi sasa.

Katika uchunguzi wake, mwandishi wa habari hii amebaini ujumbe unaotumwa kwa watu wa karibu na mkopaji ni pamoja na unaosomeka, "Ndugu wa karibu, jamaa, rafiki, jirani wa... (jina la mkopaji na namba zake za simu) aliyechukua mkopo kwa njia ya mtandao kupitia App ya… (wanataja jina la mkopeshaji), unafahamishwa kuwa mtu huyu amekiuka makubaliano kwa kutolipa deni siku husika ya marejesho na kutopokea simu za ofisi, hivyo tutamchukulia hatua kwa kosa hilo.

"Unaombwa kumpigia simu mhusika na kumjulisha kuwa ana saa mbili za kulipa deni kabla hatua kali hazijachuliwa dhidi yake. Fanya hivyo kuepuka usumbufu."

Ni ujumbe unaotumwa kwa watu wa karibu na mkopaji ukiwa na lengo la kuwataka wawe sehemu ya kumshinikiza mdaiwa kulipa deni lake.
 Kitendo hicho ni ukiukwaji wa Kanuni za Ukusanyaji Madeni Toleo la Mwaka 2019 la Kanuni za Huduma Ndogo za Fedha (Ibara ya 56 (1) (c) na (d).

Kanuni zinakataza kumtisha au kutumia nguvu au njia zisizo halali katika kukusanya au kufuatilia deni, pia kutotumia lugha inayofedhehesha au isiyofaa.

Rashidi Mazengo Mkazi wa Mbagala, Dar es Salaam, anasema aliomba mkopo mtandaoni, aliambiwa anapaswa awe na namba ya kitambulisho cha uraia.

 "Pia niliambiwa niwape namba za simu za watu wawili ambao watanidhamini na kisha baada ya kukamilisha utaratibu huo ningewekewa fedha.

"Walichukua namba za watu wangu wa karibu, wakaanza kuwatumia ujumbe mfupi kila mtu mwenye namba yangu, hii haijakaa sawa kwa sababu ni kuniaibisha," analalama.
 Mkopaji mwingine Neema Mmegelwa, mkazi wa Mbagala Zakiem, anasema alikopa Sh. 40,000 zilizogeuka shubiri, hata akakimbia makazi yake.

 "Kama ni ujumbe wa kukumbushwa kuwa ninadaiwa, nitumiwe mimi, siyo watu wenye namba yangu. Iweje leo nianze kutangazwa? Kwanini shida yake iwe tabu kwa watu wengine?

 "Niliwahi kufuatwa mpaka nyumbani kwangu, ninaamka asubuhi, ninakuta gari lipo uwanjani wanataka fedha zao. Vitisho vingi, kila siku unatumiwa meseji inasema 'tunapeleka taarifa zako kwa Jeshi la Polisi', mara 'utajuta tutakachokufanyia', anasema Neema.

 Jackson Mwalongo, dereva wa bodaboda mkoani Dar es Salaam, anasema kuwa wakati anakopa, hakujua kama wanatuma ujumbe kwa watu pindi anapochelewesha marejesho.

 "Nimekopa Sh. 120,000, nililipa Sh. 50,000 nikapitiliza kulipa. Wakawa wanapiga simu, kila nikiwaelewesha hawanielewi, mwisho nikaamua kutopokea simu zao. Cha ajabu, ninapigiwa simu na watu tofauti kuwa ninadaiwa, tena wananitukana," anasema Mwalongo.

 Zuhura Ramadhani, mkazi wa Magomeni, wilayani Kinondoni, anaonya watu kutoingia katika mifumo ya mikopo hiyo hata kama wana shida kwa kuwa inafedhehesha hadi kwa watu ambao unawaheshimu.
 "Sina hamu na mikopo ya mitandao, wametuma ujumbe hadi kwa wakwe zangu, ninaonekana mdaiwa sugu na sijui namba za hao watu wametoa wapi wakati sijawapa namba," analalama Zuhura.

 Subira Malenda, mkazi wa Mtongani, Dar es Salaam anasema alipopigiwa simu ya kulipa deni, aliwaambia kuwa atalipa ingawa amepitiliza siku moja. Mrejesho kutoka kwao ukawa "tutakukomesha". Wakatuma ujumbe kwa ndugu na jamaa zake kwamba ni mdaiwa sugu.

Latifa Mohamed anasema, "Nilichukua mkopo, nikalipa mara nne, kiwango kikapanda hadi Sh. 260,000, kipanda hadi Sh. 320,000 na ya nne ikafika 376,000.

"Yaani ukichelewa hata siku moja tu, wanakupigia simu unawaambia 'nitalipa baada ya siku mbili na riba', wanakutukana. 'Ulipokuja kwetu ulikuwa mwembamba sasa umenenepa, unaleta dharau'. Unapigiwa simu na zaidi ya watu 40, unatukanwa matusi makubwa makubwa.

"Wanaingilia hadi mawasiliano yako, wanatuma ujumbe kuwa 'huyu ni tapeli, amekopa kwenye kampuni yetu, tunaomba ulipe, maana wewe ni mdhamini wake, tunaliambia Jeshi la Polisi limkamate'.

"Ndugu wanachanganyikiwa, wanafamilia, wakwe, mimi baba yangu alinipigia, akiniambia 'umeshaanza kuwa tapeli?'" anasema.
 Latifa anasema aliamua kufunga akaunti yake ya Google, akatupa laini ya simu aliyotumia kukopa, hawakumpata tena kwa simu.

"Kabla ya hapo, waliunda kundi la WhatsApp, wakaweka kitambulisho changu cha NIDA, picha yangu, wakaungisha namba za simu zilizokuwa kwenye 'phone book' yangu kisha wakatangaza kuwa 'huyu ni tapeli'.
 "Riba yao ni kubwa, umekopa Sh. 200,000 unalipa hadi Sh. 320,000. Kuna shida nyingine, Kwa mfano, kampuni ya Pesa X nilikopa Sh. 250,000, wakanipa 80,000 ya ziada na baada ya siku tatu wakanipigia 'ukirudisha unapata mara mbili ndani ya saa 24, nikalipa wakanipa mara mbili, baada ya kuchelewa siku mbili, niliwaomba wanipe muda zaidi, ndipo matusi yalianza," anasimulia.

 Mjumbe wa Serikali ya Mtaa wa Maji Matitu C, Mbagala, Dar es Salaam, Rashidi Matimbwa anasema aliwahi kushughulisha migogoro miwili ya watu waliokopa mtandaoni, akiwa na ushuhuda wa baadhi ya wananchi walioamua kuhama eneo hilo kutokana na kero ya madeni na udhalilishaji.

"Shida iliyopo ni kwamba wengi wanaona ni rahisi kukopa mtandaoni, lakini kudaiwa wanaona kero. Hii imechangiwa pia na namna wao wanavyodai madeni yao, kwa sababu hata jinsi wanavyodai inakuwa shida," anasema.

 Mjumbe mwingine wa Kata ya Kibonde Mbagala, Veronica Mbunde anasema si mgeni wa kinachowasibu wanaokopa mtandaoni, akiwa na ushuhuda wa jirani yake aliyekumbana na vitisho vya wakopeshaji baada ya kukopa na kushindwa kurejesha kwa wakati.

 Anasema wakopaji wengi wa mtandaoni hawana elimu ya kutosha kufahamu madhara ya mikopo na nini wafanyie fedha hizo, akisisitiza jambo hilo ni hatari kwa wakopaji.

*ITAENDELEA KESHO