Wadau usafirishaji, utalii watakiwa kutunza mazingira

By Jenifer Gilla , Nipashe
Published at 04:59 PM Oct 22 2024
Naibu Waziri wa Uchukuzi, David Kihenzile.
Picha:Mpigapicha Wetu
Naibu Waziri wa Uchukuzi, David Kihenzile.

WADAU wa usafirishaji na utalii nchini wamekumbushwa kuhakikisha kuwa maendeleo ya sekta hizo hayasababishi uharibifu wa mazingira nchini.

Alisema hayo mwishoni mwa wiki na Naibu Waziri wa Uchukuzi,  David Kihenzile, wakati akifungua  Mkutano Mkuu wa Usafirishaji  na Mkutano wa Mkuu wa Mwaka wa Chama cha Mawakala wa Usafiri Tanzania (TASOTA), jijini Dar es Salaam. 

Tukio hilo la siku mbili linawaweka pamoja wadau wakuu kutoka sekta za usafiri na utalii kwa ajili ya majadiliano ya kina na kubadilishana mawazo namna ya kuendeleza sekta ya utalii nchini. 

Kihenzile alisema usafiri na utalii ni miongoni mwa sekta muhimu nchini na zima wajibu wa kuhakikisha ukuaji wake ni endelevu usioathiri mazingira.  

“Ukuaji wa sekta ya usafiri na utalii lazima uendane na uendelevu.  Ni wakati ambapo masuala ya mazingira si ya pili tena lakini yanachukuliwa kama sehemu ya msingi ya mikakati ya biashara,” alisema. 

Aidha, aliwaelekeza wadau wa sekta hiyo kuonyesha mfano kwa kuwekeza kwenye  utalii endelevu na unaowajibika kama vile   kujenga  mazoea endelevu ya kuanzisha mipango ya kupunguza utoaji wa hewa
“Uwezo wa utalii wa Tanzania ni mkubwa, na tuna kila fursa yakujiweka  katika jukwaa la kimataifa kwa kukumbatia mada hii ya uvumbuzi, ukuaji na uendelevu,” alisema. 

Alisema ni  matumaini yake  kwamba, mijadala katika kongamano hilio itaweka  msingi wa mikakati ambayo sio tu inachochea ukuaji wa sekta ya utalii ya Tanzania bali pia kuhakikisha ukuaji huu unakuwa jumuishi endelevu na  kibunifu.

Mwenyekiti wa TASOTA, Agnes Rwegasira,  alisema wamejipanga kushirikiana na serikali na mashirika binafsi  kukuza utalii wa ndani na nje kwa kufuata sera za nchi. 

Aidha, alisema majadiliano katika kongamano hilo yamejikita katika ubunifu wa teknolojia na mbinu mbalimbali kama vile kuboresha hoteli, mashirika ya usafiri na waelekezi wa watalii.