Changamoto mafuriko Jangwani yapatiwa mwarobaini

By Maulid Mmbaga , Nipashe
Published at 07:14 PM Oct 22 2024
Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) Mohamed Besta, na wawakilishi wa Kampuni ya China Communications Construction Company Limited, wakisaini mkataba wa ujenzi daraja la Jangwani, leo.
Picha Maulid Mmbaga.
Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) Mohamed Besta, na wawakilishi wa Kampuni ya China Communications Construction Company Limited, wakisaini mkataba wa ujenzi daraja la Jangwani, leo.

SERIKALI imesaini mkataba na Kampuni ya China Communications Construction Company Limited kwaajili ya utekelezaji wa ujenzi wa daraja la Jangwani mkoani Dar es Salaam lenye urefu wa mita 390, hatua itakayosaidia kuwaondoshea wananchi adha ya mafuriko iliyowakabili kwa muda mrefu.

Akizungumza leo mkoani Dar es Salaam wakati wa hafla ya kusaini mkataba huo Waziri wa Ujenzi Innocent Bashungwa, amesema ujenzi wa daraja hilo utakaojumuisha pia na barabara ya maingilio yenye jumla urefu wa mita 700, ni moja ya miradi ambayo inatekelezwa na serikali kupitia programu ya uendelezaji wa bonde la msimbazi.
 
Amesema ujenzi huu unaotarajiwa kuanza Januari mwakani utagharimu jumla ya Sh. Bilioni 97.1 na litajengwa kwa miezi 24, na kwamba utawaondolea wananchi kero ya usafiri wa barabarani kutokana na eneo la Jangwani kukumbwa na mafuriko yanayojirudiarudia na kusababisha kutopitika pindi mvua zinaponyesha.
 
“Napenda kusisitiza kuwa gharama za ujenzi wa daraja hili ni kubwa, hivyo tuzingatie thamani ya fedha ya miradi (Value for Money) wakati wa ujenzi. Naiagiza TANROADS kusimamia miradi hii kwa uthabiti mkubwa, ili barabara hii ijengwe kwa uimara na viwango vya ubora kama ilivyosanifiwa,” amesema Bashungwa.
 
Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) Mohamed Besta, ameishukuru serikali kwa kutoa fedha za ujenzi wa mradi huo, akiahidi kwamba watasimamia utekelezaji wake na kuhakikisha kuwa unazingatia viwango vya kiufundi (Technical Standards) na unakamilika kwa wakati.
 
“Nitoe wito kwa mkandarasi kufanya kazi yake kwa weledi wa hali ya juu ili kazi zikamilike ndani ya muda uliopangwa kwa viwango na gharama zilizokubalika,” amesisitiza Besta.