Milioni 3.4 waandikishwa Dar

By Maulid Mmbaga , Nipashe
Published at 07:23 PM Oct 22 2024
Katibu wa NEC, itikadi na uenezi wa CCM Amos Makala.
Picha: Maulid Mmbaga
Katibu wa NEC, itikadi na uenezi wa CCM Amos Makala.

CHAMA cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Dar es Salaam kimefanikiwa kuandikisha katika daftari la wakazi wananchi milioni 3,480,630 sawa na asilimia 96.7 huku malengo yakiwa ni wananchi milioni 3,599,247.

Akizungumza leo Katibu wa CCM Mkoa wa Dar es Salaam, Elius Mpanda, amesema katika uendeshaji wa zoezi hilo lililoanza Oktoba 11 hadi 20, mwaka huu, walifanya hamasa kubwa kwa kushirikiana na viongozi mbalimbali wa chama hali iliyofanikisha kufikia mafanikio hayo.

Amesema katika mgawanyiko wa idadi ya walioandikishwa Wilaya ya Ilala ni milioni 1,404,300, Kinondoni 653,318, Temeke 888,557, Ubungo 750,196, na Kigamboni 188,106.

Naye, Katibu wa NEC, itikadi na uenezi wa CCM Amos Makala, amewapongeza viongozi wote wa kichama kuanzia wa mkoa hadi mabalozi kwa kufanikisha zoezi hilo kufanyika kwa mafanikio makubwa.

"Pia niwashukuru wananchi kwa kutoa ushirikiano katika suala la uandikishaji, ni faraja kubwa kwa CCM kuona kwamba mumefanikiwa kuandikisha kwa asilimia 96.7, hii inaonyesha namna wananchi walivyo na muamko katika kuchagua viongozi," amesema Makala.