Rukwa, Morogoro yaongoza matukio ya ulaghai mtandaoni

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 08:28 PM Oct 22 2024
Rukwa, Morogoro yaongoza matukio ya ulaghai mtandaoni
Picha:Mtandao
Rukwa, Morogoro yaongoza matukio ya ulaghai mtandaoni

RIPOTI ya Tathimini ya Mawasiliano Tanzania ya Juni hadi Septemba,2024 imeonyesha mkoa wa Rukwa na Morogoro iliongoza kwa kuwa na majaribio ya ulaghai.

Aidha,imebainisha kuwa matukio ya ulaghai yamepungua kwa asilimi 28, ikilinganishwa na yaliyoripotiwa katika ripoti ya Juni 2024 huku mikoa hiyo ikiongoza mwaka mzima.

Ripoti hiyo ambayo hutolewa hivi karibuni na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kwa kila miezi mitatu, imeonesha mikoa hiyo imeongoza kwa kuwa na theluthi moja ya majaribio ya ulaghai nchini.

Aidha, mkoa wa Mbeya (1,112) ,Dar es Salaam (959) na Arusha (351) zilifuata kwa majaribio hayo kwa zaidi ya asilimia moja hadi 10.

"Kila mwaka kwenye ripoti zetu mikoa ya Rukwa na Morogoro imekuwa na matukio mengi ya ulaghai,"amesema Mkurugenzi wa Masuala ya Kisekta wa TCRA, Mhandisi Felician Mwesigwa leo wakati akiongea na waandishi wa habari.

Amesema katika mkoa wa Rukwa wilaya zilizoongoza na matukio yake kwenye mabano ni Simbawanga (5,198), Nkasi (250) na Kalambo (122); huku mkoa wa Morogoro ni Ifakara (3,922), Kilombero (1,306), Morogoro (127), Kilosa( 89), Ulagha (21), Mvomero (10), Malinyi (8) na Gairo (3).

Akifafanua kwanini mikoa hiyo,amesema hayo ni matukio ya ulaghai ambayo chanzo chake kilikuwa kwenye mikoa hiyo, kwamba waliojaribu hivyo walitekeleza wakiwa eneo hilo.