Waacheni watoto wa kike watimize ndoto zao msiwazalishe mapema

Nipashe
Published at 11:57 AM Jul 16 2024
Rais Samia Suluhu Hassan.
Picha: IKULU
Rais Samia Suluhu Hassan.

WAKATI Rais Samia Suluhu Hassan akiwa ameanza ziara yake katika Mkoa wa Katavi kukagua shughuli mbalimbali za maendeleo na kuzindua miradi, pia ametembelea Hospitali ya Rufani Mkoa wa Katavi na kushuhudia watoto waliojaa hospitalini hapo wakiwa wamejifungua watoto wenzao.

Kwa mshtuko Rais Samia, alishuhudia wengi wa wazazi kwenye wodi hiyo wakiwa na umri kati ya miaka 15 na 19.

Ukiangalia umri huo ni wa watoto ambao wanapaswa kuwa shuleni, lakini ndoto zao zimezimwa na sasa wamekuwa wazazi wa kulea watoto wenzao.

Kujifungua mtoto ukiwa na umri mdogo kuna athari nyingi kwa sababu viungo vinakuwa havijakomaa na wengi wao huishia kufanyiwa upasuaji kutokana na kushindwa kuhimili mikikimikiki ya uzazi.

Athari nyingine ni kuchanika kwenye njia ya uzazi na matokeo yake kupata tatizo la ugonjwa wa fistula.

Wataalamu wengi wa afya wanaamini kuwa umri sahihi wa mwanamke kupata ujauzito ni kuanzia miaka 20 hadi 35 ambapo viungo vyake vinakuwa vimeshakomaa.

Hata hivyo, watoto wengi wa kike hasa wa vijijini wanalazimika kujifungua katika umri mdogo kwa kujiingiza katika mahusiano wakiwa katika umri mdogo au wengine kulazimishwa ndoa za utotoni na wazazi.

Wengine hupata mimba kwa kubakwa na kulazimika kupata mtoto akiwa na umri mdogo. Matukio ya mabinti kuzaliwa katika umri mdogo yanaathiri ndoto zao za kufikia maisha wanayoyapenda wakiwa wakubwa.

Sheria ya Ulinzi wa Mtoto, 2009 inazuia mtoto (umri chini ya miaka 18) kutekeleza majukumu ya mtu mzima. 

Aidha, Sheria ya Ndoa ya Mwaka 1971 inamzuia mtoto chini ya miaka 15 kuolewa na sheria hii ilikuwa na lengo la kumlinda mtoto asipewe majukumu ya kulea familia akiwa na umri mdogo.

Rais Samia alipotembea Hospitali ya Katavi, alibaini kuwa ni mama mmoja tu ndiye aliyepevuka ambaye alikuwa na miaka 22, lakini wengine wote walikuwa kati ya miaka 15 na 19 na hao walikuwa wamejifungua watoto ambao hawajatimiza siku zao za kuzaliwa (njiti).

Kwa kuonesha kusikitishwa na alichokikuta, aliwaomba wananchi wa Mkoa wa Katavi, kuwapa nafasi watoto wa kike waweze kusoma na kutimiza malengo yao na hata wafikie umri unaostahili angalu ajifungue akiwa amefikia umri wa miaka 19 na kuendelea, lakini sio kwa hali aliyoikuta hospitalini hapo.

“Ujumbe huu ni kwenu wananchi mliopo hapa na wale ambao wananisikiliza kupitia vyombo vya habari, tujitahidi kuwapa nafasi watoto wa kike wapate elimu, wapevuke kabla ya kuolewa au kupewa ujauzito, hilo ninaomba sana sana.”

Ushauri na ombi alilotoa Rais Samia ni amri ambayo inatakiwa itekelezwe kote nchini, kwa sababu vitendo vya kukatisha ndoto za watoto wa kike kuendelea na masomo vimekuwa vikifanyika sana katika mikoa ya Kanda ya Ziwa na mikoa ya Kusini.

Changamoto wanayokutana nayo wazazi hao wadogo ni kutelekezwa na watu waliowazalisha na kuwaachia mzigo wa malezi wazazi wa watoto hao ambao nao wengi wao hawana uwezo.

Matokeo yake ni watoto kupata utapiamlo na udumavu kwa kukosa chakula bora.

Watoto wa kike waachwe wasome, wasizalishwe wakiwa wadogo, waacheni watimize ndoto zao.