KIONGOZI wa Mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa, Godfrey Mzava, amesisitiza matumizi ya mfumo wa kidigitali katika kuwapata wazabuni kwenye miradi mbalimbali na kuondoa malalamiko kwa waombaji.
Amesema Serikali imeendelea kutoa fedha nyingi kwenye miradi ya barabara lengo likiwa ni kurahisisha usafiri kwa wananchi kwenda kwenye maeneo ya huduma za kijamii.
Kadhalika amesema Rais wSamia Suluhu Hassan ameendelea kuelekeza manunuzi yote ya Umma yapitie kwenye mfumo wa manunuzi wa kidigitali
Amesema mfumo huo unasaidia wazabuni kuingia kwenye mfumo ambao wenyewe unawachakata na kumpa zabuni mtu ambaye ana sifa zote za kupata ile za buni na ambaye hana sifa mfumo moja kwa moja unamtoa nje ya utaratibu.
"Ni mfumo ambao umeondoa malalamiko kwasababu kuna baadhi ya watu wamekuwa na malalamiko wanapewa zabuni wengine wao wanaachwa huku wakiwa na sifa zinazotakiwa,".
"Watu wanakutana mezani wanamalizana kwenye meza pale wanapeana zabuni, lakini kupitia mfumo huu wa udhibiti wa manunuzi ya umma kwenye masuala ya zabuni sasa hakuna kukutana mezani," ameaema.
Amesema lengo ni kudhibiti, kuhakikisha kwamba manunuzi ya Umma yote yanakwenda sawa sawa na jinsi ambayo ineelekezwa Ili kuhakikisha kwamba hakuna hujuma na ubadhilifu unaofanyika.
"Na tumefarijika kwamba ndugu zetu hawa wa TARURA wametumia mfumo huo vizuri na mradi umetekwlezwa kama ilivyolengwa" amesema.
Mradi huo wa Barabara ya mita 300 kuelekea Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha unaosimamiwa na Wakala wa Barabara za Mjini na Vijijini (TARURA) umejengwa kwa gharama ya sh.milion 495.8 fedha kutoka Serikali kuu na mpaka sasa sh. Miln 490,018,125 zimetumika.
Awali akipokea Mwenge wa Uhuru kutoka Wilaya ya Bagamoyo , Mkuu wa Wilaya ya Kibaha Nickson John amesema Mwenge huo utapita miradi 28 yenye thamani ya sh. Trillion 8.5 .
Katika Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha Mwenge wa Uhuru umepitia katika mradi wa jengo la wagonjwa wa nje katika Zahanati ya Vikuruti, kituo cha wanafunzi wenye mahitaji maalumu shule ya Msingi Mlandizi, shughuli za mradi wa mapambano dhidi ya Malaria, shughuli za mapambano dhidi ya Ukimwi.
Miradi mingine ni kongani ya viwanda ya Sino Tan, ujenzi wa vyumba vya madarasa na matundu ya vyoo shule ya Msingi Kilangalanga, shamba la mradi wa miti shule ya Sekondari Kawawa na mradi wa maji Kijiji Cha Ruvu stesheni ambao unasimamiwa na Mamlaka ya maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA).
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED