ACT yataka sheria kandamizi vyombo vya habari zifutwe

By Elizabeth Zaya , Nipashe
Published at 09:42 AM May 21 2024
 Waziri Kivuli wa Mawasiliano, Teknolojia ya Habari na Uchukuzi wa chama hicho, Rahma Mwita.
Picha: Mpigapicha Wetu
Waziri Kivuli wa Mawasiliano, Teknolojia ya Habari na Uchukuzi wa chama hicho, Rahma Mwita.

CHAMA cha ACT-Wazalendo kimeitaka serikali kufuta sheria zote kandamizi na zinazopora uhuru wa vyombo vya habari na kutengeneza mpya kwa kushirikiana na wadau, zitakazolenga kuleta uhuru, weledi na ukuaji wa sekta ya habari nchini.

Aidha, kimeitaka serikali isimamie uanzishwaji wa Baraza Huru la Habari nchini ili kulinda na kutetea haki na maslahi ya wanahabari nchini.

Kauli hiyo ilitolewa jana na Waziri Kivuli wa Mawasiliano, Teknolojia ya Habari na Uchukuzi wa chama hicho, Rahma Mwita, wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, ikiwa ni uchambuzi wa bajeti ya wizara hiyo iliyosomwa bungeni juzi na waziri mwenye dhamana, Nape Nnauye.

“Katika miaka saba iliyopita, Tanzania imetunga sheria kadhaa zinazozuia uhuru wa vyombo vya habari, uhuru wa kujieleza na zinazokazia ukali wa sheria zilizopo ambazo ni vikwazo katika kuhabarisha wananchi,” alisema Rahma.

“Sheria hizi ni pamoja na ile ya kupata habari ya mwaka 2016, kanuni za maudhui ya mtandaoni 2018, Sheria za makosa ya kimtandao 2015, Kanuni za jumla za 2016, na Sheria ya Takwimu 2015 pamoja na marekebisho yaliyofanywa kwa mujibu wa Sheria ya Mabadiliko ya Sheria Mbalimbali Na. 3 mwaka 2018. Kwa pamoja, sheria hizi zinajinaisha uandishi wa habari za kina na za uchunguzi na zilikazia ukali wa sheria zilizopo ambazo ni vikwazo katika kuhabarisha wananchi.”

“Tumeona Bunge la Jamhuri limepitisha mabadiliko ya Sheria ya Huduma za Habari ya mwaka 2016, Sura 229, lakini wadau wamelalamikia mambo kadhaa katika mchakato wa mabadiliko hayo kama vile mtindo uliotumika kuwasilisha mabadiliko hayo ambao ni mabadiliko ya sheria mbalimbali, jambo ambalo limefanya muswada huo kama jambo la jumla na si jambo mahususi linalohitaji mjadala mkubwa na maafikiano ya wadau.”

Rahma alisema jambo jingine ni lugha iliyotumika na mchakato wa mabadiliko ulivyofichwa huku sehemu kubwa ya wadau wakishindwa kushiriki kwa sehemu kubwa kwenye mabadiliko hayo jambo ambalo bado yanaminya uhuru wa habari nchini.

Kuhusu deni la serikali kwenye vyombo vya habari, ACT-Wazalendo kiliitaka serikali kupitia bajeti kuu kuzingatia madai hayo na kutenga angalau asilimia 0.4 ya bajeti kwa ajili ya wizara ya habari, ili iweze kulipa madeni hayo kwa mkupuo.

MAWASILIANO

Kadhalika, chama hicho kiliitaka serikali kufanya marekebisho ya kanuni zinazosimamia vifurushi vya dakika za kupiga, mitandao ya intaneti na meseji ili kushusha gharama zake na kuongeza ushirikishwaji wa wananchi kuwezesha kudhibiti, uholela wa kampuni hizo kupandisha gharama hizo.

Kilisema katika hotuba ya bajeti ya serikali, waziri hakuzingatia wala kutoa hatua za kibajeti katika kushughulikia masuala hayo makubwa ya gharama za vifurushi na upatikanaji wa data na kwamba kuna haja ya serikali kuanzisha mchakato wa kutengeneza upya sera ya taifa ya mawasiliano.

Kilipendekeza ni vema mchakato huo ukawashirikisha watoa huduma, watumia huduma, wataalamu wa masuala ya kimtandao na wadau wengine.

Kuhusu kukatika nyaya za baharini, kiliitaka serikali kuwekeza kwenye njia mbadala ya satellite na kwenye utafiti wa anga ili kujitegemea kimtandao kwa ajili ya usalama wa taifa na kuitaka kuzisimamia kampuni za kutoa huduma za mitandao kutoa fidia kwa watumiaji kwa muda ambao shughuli zao zilisimama kutokana na tatizo la mtandao.

Pia kimetaka serikali itoe huduma ya data bure maeneo yote ya umma kama vile hospitali, shuleni, vyuoni, ofisini na maeneo ya masoko, kupunguza gharama za kodi katika miundombinu ili mtumiaji apate nafuu ya kupata huduma.

Rahma alisema serikali ina wajibu wa kuratibu na kusimamia huduma za mawasiliano ya simu na intaneti zikiwamo viwango vya uwekezaji, ubora na viwango wa huduma, gharama za huduma za uzalishaji na usambazaji.

Aidha, alisema katika mazingira ambayo sekta hii inakua kwa kasi bila kuratibu na kusimamia vizuri viwango vya huduma na gharama zake ni kuruhusu wananchi kunyonywa na kupitia mateso makubwa bila uangalizi.

Vile vile, kuna haja ya serikali kuanzia mwaka huu na miaka mitano ijayo kuwa na Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) ambao unatengewa fedha za kutosha ili kuimarisha mtandao wa mawasiliano nchini.

MATAPELI

Kuhusu wimbi la utapeli mitandaoni, chama hicho kilisema kuna haja serikali ikashirikiana na wizara pamoja na taasisi nyingine kutambua biashara za mtandaoni kisheria ili kupunguza wimbi la utapeli.