Wakulima waeleza utamu wa mradi wa AID-I

By Godfrey Mushi , Nipashe
Published at 11:24 AM Dec 31 2024
Wakulima waeleza utamu wa mradi wa AID-I
Picha: Mtandao
Wakulima waeleza utamu wa mradi wa AID-I

MRADI wa kupeleka teknolojia haraka kwa wakulima (AID-I), unaotekelezwa na Shirika la Floresta Tanzania, kwa kushirikiana na World Vegetable Center, umeanza kuonyesha matunda, baada ya wakulima kueleza namna wanavyoridhishwa na upatikanaji wa mbegu na miche bora ya mboga.

Licha ya kurahisisha upatikanaji wa mbegu, pia umewasaidia wakulima kuimarisha mnyororo wa thamani wa mazao ya mboga, matunda, viungo na kuboresha lishe ya jamii.

Wakizungumza jana katika Kijiji cha Embukoi, Kata ya Donyomoruwa, Wilaya ya Siha, mkoani Kilimanjaro, Lekishon Mollel, ambaye ni mwenyekiti wa viongozi wa mila wa wafugaji wa jamii ya Kimasai (Leigwanani), alisema kutatuliwa kwa changamoto hiyo kunaongeza tija na ufanisi wa kuwa vyanzo vya uhakika vya usalama wa chakula.

“Kwa mfano leo ukiangalia maeneo yote ya ukanda huu, hakuna malalamiko ya wakulima kukosa mbegu na miche bora ya mboga. Kupitia mradi huu, sasa wamasai wanakula mlo kamili, unaojumuisha mboga na matunda na hivyo kupambana na changamoto za lishe duni miongoni mwa jamii, hasa kwa vijana balehe,” alisema Mollel.

Mwenyekiti wa kikundi cha wakulima cha kuweka na kukopa cha Emusoi, Jackson Laizer, alisema wanayaona mabadiliko makubwa katika lishe kwenye jamii yao, kwa kuwa Shirika la Floresta Tanzania, limewaelimisha wafugaji wa kimasai kula mboga.

Mradi huo wa AID-I), unafadhiliwa na Shirika la Misaada la Watu wa Marekani (USAID).

Mkurugenzi wa Shirika la Floresta Tanzania, Richard Mhina, alisema mradi huo wa AID-I, unalenga kuwafikia watu 5000 kutoka Mkoa wa Kilimanjaro, ambapo asilimia 60 ni vijana na asilimia 40 ni watu wazima.

Aidha, alisema mradi huo sio tu unalenga kuongeza uwezo wa kiuchumi wa makundi hayo, bali pia kuwezesha vijana na wanawake kuwa wahamasishaji wakuu wa sekta ya kilimo na maendeleo ya kijamii.

Mradi wa AID-I, ni sehemu ya mpango wa kimataifa chini ya msaada wa Serikali ya Marekani (USAID) wa kukabiliana na njaa na umasikini, ukilenga zaidi kutoa msaada kwa wakulima wadogo katika nchi za Tanzania, Malawi na Zambia, kuhakikisha wanapata teknolojia, ubunifu na taarifa zinazohitajika haraka ili kuongeza na kuimarisha uzalishaji wa chakula.

Aidha, Mhina, alisema mradi huo wa AID-I, unalenga kuwafikia watu 5,000 kutoka Mkoa wa Kilimanjaro, ambapo asilimia 60 ni vijana na asilimia 40 ni watu wazima.

Aidha, alisema mradi huo siyo tu unalenga kuongeza uwezo wa kiuchumi wa makundi hayo, bali pia kuwezesha vijana na wanawake kuwa wahamasishaji wakuu wa sekta ya kilimo na maendeleo ya kijamii.