JUMLA ya wachezaji 28 wameitwa kwenda kuunda kikosi cha Timu ya Tanzania Bara, Kilimanjaro Stars, kitakachoshiriki michuano ya Kombe la Mapinduzi inayotarajiwa kuanza Januari 3, mwakani, kwenye Uwanja wa New Amaan, Zanzibar.
Kikosi hicho kitakuwa chini ya Ahmad Ally, ambaye naye kwa mara ya kwanza, ameteuliwa kuwa Kocha Mkuu wa kikosi hicho.
Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, kocha huyo ambaye ni Kocha Mkuu wa JKT Tanzania, alisema amepata furaha isiyo kifani kwani hajawahi kuifundisha timu yoyote ya taifa kwenye historia yake kisoka.
Alisema kuteuliwa kwake kunaonesha imani kubwa kwake, ambapo kupitia kikosi hicho ataendelea kujifunza, lakini pia atakuwa ametengeneza wasifu mkubwa kwani ni ndoto ya kila mwalimu kuifundisha timu ya taifa.
"Kusema kweli mimi binafsi sikutarajia hili kwa wakati huu, imekuwa ni 'sapraizi', jana (juzi), ndiyo nipewa taarifa rasmi ya kukifundisha kikosi hicho, baada ya hapo tukakaa na Idara ya Ufundi ya Shirikisho la Mpira wa Miguu (TFF), kutengeneza kikosi hiki, na tuliangalia malengo ambayo ni kutengeneza uwezo wa vijana ambao watakwenda kucheza AFCON 2027 na kuchukua wachezaji wa timu ya taifa ambao hawapati nafasi mara kwa mara ya kucheza ili nao waweze kupata nafasi kwenye michuano hii ya Mapinduzi kwani huko mbele tuna michuano ya CHAN pamoja na AFCON 2027," alisema kocha huyo.
Walioitwa kuunda kikosi hicho, ni Metacha Mnata na Ayoub Lyanga wa Singida Black Stars, Ramadhani Chalamanda, Said Naushad na Hijja Shamte kutoka Kagera Sugar, Antony Mpemba, Lusajo Mwaikenda, Paschal Msindo, Sospeter Bajana, Abdulkarim Kiswanya, Idd Selemani 'Nado', Nassor Saadun, na Abdul Hamisi Sopu, wote kutoka Azam FC.
Wengine ni Nickson Mosha na Ahmed Pipino wa KMC, Vedatus Masinde kutoka TMA, Lameck Lawi, Semfuko Charles na Bakari Msimu wote wakitokea Klabu ya Coastal Union, Wilson Nangu, Gamba Idd na David Brayson wa JKT Tanzania.
Wachezaji wengine walioitwa ni Zidane Sereri wa Dodoma Jiji, William Edgar wa Fountain Gate, Offen Chikola kutoka Tabora United, Joshua Ibrahim wa KenGold, Sabri Kondo wa KVZ na Crispin Ngushi kutoka Mashujaa FC.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED