Sheikh wa Mkoa wa Arusha, Shaaban Abdallah, amewataka viongozi wa dini kuunga mkono juhudi za Rais Samia Suluhu Hassan katika kuhimiza matumizi ya nishati safi kwa lengo la kulinda mazingira na kuhakikisha ustawi wa kizazi cha sasa na kijacho.
Akizungumza leo wakati akialika viongozi wa taasisi mbalimbali za Kiislamu kushiriki katika tukio kubwa la uhamasishaji wa matumizi ya nishati safi, Sheikh Shaaban ametoa pongezi maalum kwa Mbunge wa Jimbo la Arusha Mjini, Mrisho Gambo, kwa juhudi zake za kusisitiza suala hilo muhimu.
“Sheikh Gambo ameonyesha mfano mzuri kwa kumwalika Mufti wa Tanzania, Sheikh Abubakar Zubeir, kushiriki katika kongamano la nishati safi litakalofanyika Januari 11, 2025, jijini Arusha,” amesema Sheikh Shaaban na kuongeza kuwa hatua hiyo ni ya kuigwa na viongozi wengine.
Sheikh Shaaban amewaalika viongozi wa taasisi mbalimbali za Kiislamu zikiwemo Baraza la Kiislamu Tanzania (BAKWATA), Twariqatul-Qadiriya-Raziqiya Al-Jaylaniya, Arusha Muslim Center, Bohora, Arusha Muslim Union, Mtendeni, Shia, Ansaar Muslim Youth Center-Kanda ya Kaskazini, Ismailia Chairman, Quadiriya, na Arusha Islamic Center kushiriki katika hafla hiyo.
“Hafla hii ni fursa muhimu ya kuhamasisha na kutoa elimu kuhusu matumizi ya nishati safi ya kupikia. Ushiriki wa viongozi wa dini ni muhimu kwa kuwa jamii itapata uelewa wa kina kuhusu faida za nishati safi kwa mazingira na afya,” amesisitiza Sheikh Shaaban.
Hafla hiyo inatarajiwa kufanyika jijini Arusha, ikiwa na lengo la kuhimiza matumizi ya nishati safi ili kupunguza athari za mabadiliko ya tabianchi na kuboresha ustawi wa jamii.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED