Mgombea wa nafasi ya Uenyekiti wa Baraza la Wanawake (BAWACHA) kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Sharifa Suleiman, amerudisha fomu leo katika ofisi za CHADEMA Kanda ya Pwani.
Akizungumza na waandishi wa habari baada ya kurudisha fomu hiyo, Sharifa amesema kuwa anaiomba Kamati Kuu ya chama kumpitisha ili aweze kuwatumikia wanawake kwa bidii, akisisitiza kuwa ameanza kushiriki harakati za chama tangu akiwa na umri wa miaka 18.
“Naomba ridhaa ya chama changu kwa sababu dhamira yangu ni kutetea haki za wanawake na kuhakikisha wanarudishiwa nafasi na haki ambazo wamezikosa tangu nchi yetu ipate uhuru,” amesema Sharifa.
Kwa upande wake, Glory Tausi, mgombea wa nafasi ya Naibu Katibu Mkuu BAWACHA Bara na mwanzilishi wa CHADEMA Digital, amerudisha fomu yake ya kugombea nafasi hiyo. Glory ameeleza kuwa lengo lake ni kuanzisha programu maalum za kuinua uchumi wa wanawake kupitia mafunzo ya kidijitali na uwezeshaji wa kiuchumi.
“Lengo langu ni kuleta maendeleo ndani ya Baraza la Wanawake CHADEMA. Nitahakikisha wanawake wanapatiwa mafunzo ya kidijitali na ujuzi wa kiuchumi ili wasalie nyuma katika masuala muhimu ya maendeleo,” amesema Glory.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED