Simba, Yanga wakati sahihi wachezaji 'kujinadi' sokoni

Nipashe
Published at 10:13 AM Apr 20 2024
Mchezaji  wa Simba SC, Kibu Denis akiwatoka wachezaji wa Yanga katika mchezo wao uliopita, ambao Yanga walibuka na ushindi wa goli 5-1.
Picha: Maktaba
Mchezaji wa Simba SC, Kibu Denis akiwatoka wachezaji wa Yanga katika mchezo wao uliopita, ambao Yanga walibuka na ushindi wa goli 5-1.

MECHI yoyote ya watani wa jadi wa soka, Simba na Yanga, inayochezwa hapa nchini ni kubwa bila kujali aina ya mashindano ambayo timu hizo mbili zinachuana.

Leo kwa mara nyingine watani hao wanakutana, ni katika mechi ya mzunguko wa pili wa Ligi Kuu Tanzania Bara, itachezwa kuanzia saa 11:00 jioni kwenye Uwanja wa Benjamin, Dar es Salaam.

Yanga ambao ni mabingwa watetezi, ndio vinara wa Ligi Kuu Tanzania Bara wakiwa na pointi 55, wamecheza mechi 21 na watani zao, Simba wako katika nafasi ya tatu, wameshuka dimbani michezo 20.

Azam FC , mabingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara msimu wa mwaka 2013/2014 maarufu 'Wauza Lambalamba' wao wapo katika nafasi ya pili katika msimamo wa ligi hiyo, wamejikusanyia pointi 51 kibindoni, lakini wamecheza michezo 23.

JKT Tanzania ya Dar es Salaam, Mashujaa FC kutoka Kigoma, Tabora United ya mkoani Tabora na Mtibwa Sugar ya Manungu Turiani, Morogoro ziko katika hatari ya kushuka daraja, ziko mkiani kwenye msimamo wa ligi hiyo inayoshirikisha klabu 16 za mikoa mbalimbali.

Kama ambavyo bado mbio za kuwania ubingwa wa ligi hiyo ziko wazi, kwa kila timu inayohitaji kutimiza malengo yake inatakiwa kushinda mechi zote zilioko mbele yake, pia katika vita ya kujinusuru na janga la kushuka daraja, lolote linaweza kutokea.

Huku mkiani ndio mambo hayatabiriki, tofauti ya pointi ni chache, hivyo timu hizo zinazoburuza mkia endapo 'zitapindua meza' na kupata matokeo chanya kwenye michezo yake iliyobakia, msimamo wa ligi unaweza kubadilika na wale walioamini wako mahali salama kibao kikawageukia.

Kwa maana nyingine muhimu, bado kila timu ina nafasi ya kupigania kufanya vyema kwa sababu mbali na kumaliza kwenye nafasi nzuri, itajihakikishia kupata kiasi kikubwa cha fedha zinazotolewa kama zawadi na wadhamini wenye haki ya kurusha matangazo ya televisheni.

Kuelekea mechi ya leo, ambayo ni dabi mojawapo inayozungumzwa hapa barani Afrika, matokeo yoyote ya ushindi yataifanya timu iliyovuna kujiimarisha kwenye mbio za kutwaa taji hilo kwa msimu wa mwaka 2023/2024.

Lakini kikubwa tunawakumbusha wachezaji kuupa umuhimu na heshima inayostahili mchezo huo. Wachezaji wanatakiwa kufahamu kupitia viwango watakavyovionyesha katika dabi hiyo, vitatoa mustakabali, hatima na thamani zao kuelekea msimu ujao.

Wachezaji watakaojituma na kusaidia timu zao kupata matokeo chanya, mbali na ahadi nono za fedha watakazopewa, lakini kwa kila mmoja atajitengenezea mazingira mazuri ya kuboreshwa kwa mkataba wake na wale walioko ukingoni, kufanya mazungumzo ya mkataba mpya wakiwa na nguvu.

Pia tunawakumbusha mechi ya dabi hufuatiliwa na makocha na mawakala wa ndani na nje ya Tanzania, hivyo watumie fursa hiyo vyema kujiweka sokoni na kwa wale ambao 'nyota' zao zitang'ara, klabu zao zitapokea ofa kwa ajili ya kuwasajili na maisha mapya ya soka yataanzia hapo.

Mbali na kuonyesha ufundi na  mbinu, nidhamu ni jambo muhimu linalotakiwa kuonyeshwa kwa wachezaji wa timu zote mbili kwa sababu zitawaongezea nafasi ya kuitwa katika timu za taifa lakini pia ni darasa kwa wachezaji wenzao chipukizi ambao watafuatilia mechi hiyo.

Mashabiki pia wanatakiwa kufahamu mipaka yao, wasiturudishe nyuma katika zama za kurushia wachezaji au waamuzi chupa za maji pale ambao wanapokasirishwa na matokeo au uchezeshaji.