Waziri Mavunde awaanikia hati ujenzi, kiwanda chumvi Kilwa kuanza 2025

By Grace Mwakalinga , Nipashe
Published at 11:04 AM Oct 18 2024
Shughuli za uzalishaji chumvi kienyeji Kilwa zikiendelea.
PICHA: MTANDAO
Shughuli za uzalishaji chumvi kienyeji Kilwa zikiendelea.

MWAKA 2022, wakazi wa Kilwa mkoani Lindi walipopata ugeni wa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, walimwasilishia kilio chao mkuu wa nchi, wakihitaji kiwanda cha kuchakata chumvi yao.

Rais akawakubalia kwa kuwaahidi kuwatekelezea. Miaka miwili baadaye, wakawa mashuhuda mnamo Septemba 18 mwaka huu, leo ikitimu mwezi mmoja tangu tukio hilo, wakamwona Waziri wa Madini, Anthony Mavunde akikabidhi hati ya ujenzi wa kiwanda hicho wilayani Kilwa.

“Mheshimiwa Rais alipokuja kwenye ziara yake katika mkoa huu, moja kati ya mambo aliyoyasikia na kupokea ni kilio cha wazalishaji wa madini ya chumvi na akaagiza kiwanda cha chumvi kijengwe hapa.

“Niwaambie kuwa Rais anafuatilia suala hili la wazalishaji wa chumvi na hatua hii ni utekelezaji wa ahadi yake kwenu baada ya kusikia kilio chenu,” anasema Mavunde. 

Akafafanua kwamba, hatua walioko sasa ni kusimamia maelekezo hayo ya mkuu wa nchi kuhakikisha wanasimamia ujenzi wa kiwanda hicho haraka, ili kutatua kero hiyo ya muda.

Uzalishaji wa chumvi mkoani Lindi, kihistoria  ulianza mwaka 1969 na mradi wa ujenzi wa kiwanda hicho sasa, unasimamiwa na Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) katika eneo la Lingaula wilayani Kilwa.

Waziri Mavunde, katika hafla hiyo akaiagiza STAMICO kuhakikisha kabla ya Desemba, mwaka huu ihakikishe wameandaa mafunzo ya namna bora ya kuzalisha chumvi sahihi na yenye ubora unaotakiwa, kuifanya nchi itumie zao la ndani.

Pia, akafafanua kwamba mradi wa kujenga kiwanda hicho unatarajiwa kukamilika  ifikapo Aprili mwaka ujao, 2025, hata kuifanya ahadi ya Rais ya mwaka 2022 kwa wakazi wa Kilwa inatimia, kiwanda kikisafisha madini kwa kiwango asilimia 99.5.

Mkuu wa Mkoa Lindi, Zainab Telack, ambaye ndiye alitoa ardhi panapojengwa kiwanda hicho, akasema kukamilika kwa mradi huo kutasaidia kufungua fursa sio tu kwa wakulima wa chumvi, bali wananchi wa mkoa wa Lindi kwa ujumla.

CHIMBUKO LA UZALISHAJI

Uzalishaji chumvi mkoani Lindi historia yake ilianza rasmi mwaka 1969, katika lililotajwa wilayani Kilwa, kutokana na kuwa na mazingira mazuri ya uzalishaji wa chumvi mahali hapo pwani ya Bahari ya Hindi.

Hata hivyo, uzalishaji huo kwa muda mrefu, una historia ulianza katika ubora wa chini na ukaendelea kuimarika kadri teknolojia na mbinu za uzalishaji zinavyoboreshwa.

Historia hiyo inafafana na wazalishaji chumvi wilayani Kilwa, wamekuwa wakikabiliana na changamoto za ukosefu wa soko la uhakika, teknolojia duni na bei ndogo za bidhaaa yao, wakiwa wanategemea wanunuzi wa kati, ambao mara nyingi hufanya biashara kwa gharama kubwa na chumvi yao haina viwango kimataifa, hali inayoipa thamani ndogo soko.

Waziri wa Madini, Anthony Mavunde, anasema kiwanda hicho kitasaidia kusafisha na kuongeza thamani ya chumvi inayozalishwa na wananchi, wenye kilio cha masoko na bei duni.

Wakulima wa chumvi, hasa wa Kilwa wamekuwa wakikabiliwa na changamoto kadhaa, ikiwamo kukosekana soko la uhakika, teknolojia duni na ubora wa chini wa bidhaa.

Ripoti ya Shirika la Madini ya Taifa STAMICO ya mwaka 2023, inaonyesha uzalishaji chumvi nchini, umekabiliwa na changamoto nyingi, wakulima wengi hawajafanikiwa kufikia ubora unaotakiwa katika masoko kimataifa. 

Mwenyekiti wa Chama cha Wanawake Wachimba Madini Tanzania, ambaye ni Mwenyekiti wa UWT Mkoa wa Lindi, Palina Ninje, anasema ujenzi wa kiwanda cha chumvi mkoani humo, unawapa fursa wanawake wazalisha chumvi, wanakabiliwa na changamoto za bei duni. 

Anataja faida za kiwanda hicho hasa kwa wanawake, ni manufaa ya soko, bei nzuri ya bidhaa yao, hivyo kuwaongezea kipato, sambamba na kupata mafunzo ya kuongezea thamani bidhaa yao.

“Tutanufaika si tu katika uzalishaji wa chumvi yenye viwango vya kimataifa, bali pia kuwapa uwezo wa kushiriki katika masoko ya kimataifa, kwa kuimarisha ushirikiano kati ya serikali, taasisi za kifedha na wakulima.

“Uwekezaji huu unatarajiwa kuboresha maisha ya wanawake na kuhamasisha ukuaji wa uchumi katika jamii zao,” anasema Ninje.

Waziri Mavunde ana ufafanuzi wa ziada: “Serikali pia inakusudia kushirikiana na taasisi za kifedha, ili kuwasaidia wakulima kupata mikopo nafuu kwa ajili ya kuwekeza zaidi katika shughuli zao za uzalishaji wa chumvi. Hatua hizi zote zinalenga kuboresha sekta ya chumvi nchini na kuleta mafanikio kwa wakulima wadogo.”

NGUVU YA SOKO

Kiwanda hicho cha kusafisha chumvi kitakapokamilika, kinatarajiwa kunufaisha wazalishaji kupata bei nzuri ya bidhaa zao, huku wakishiriki katika masoko  kimataifa.

Mkurugenzi wa STAMICO, Dk. Vennance Mwasse, anasema kiwanda hicho kitakapokamilika Aprili mwaka ujao, kitaweza kuzalisha tani 200,000 za chumvi kwa mwaka.

Anasema, ni hatua itakayoongeza uzalishaji chumvi nchini na kusaidia kupunguza utegemezi, pia uagizaji kutoka nje.

Ripoti ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT) inaonyesha mahitaji ya chumvi safi na ubora kimataifa, yanaongezeka kwa kasi katika masoko kimataifa, hususan Mashariki ya Kati, Ulaya na baadhi ya nchi za Asia.

Hapo kuna ushauri kitaalamu, wazalishaji chumvi nchini Tanzania, wanaweza kunufaika na soko hilo kwa kutumia kiwanda hicho cha kisasa.

Serikali imekuwa ikielekeza imepanga kuwekeza katika teknolojia za kisasa za kusafisha chumvi, zitazosaidia kuongeza uzalishaji wa chumvi yenye ubora wa kimataifa. 

TAASISI FEDHA, WAKULIMA 

Ili kuhakikisha mradi huu unatekelezwa kwa mafanikio, ushirikiano kati ya serikali, taasisi za kifedha na wakulima ni muhimu, STAMICO ikiwa na jukumu la kusimamia ujenzi wa kiwanda na kutoa mafunzo kwa wakulima. 

Mkuu wa Mkoa Lindi, Zainab Telack, anasema wanawajibika kuhakikisha mazingira bora ya utekelezaji mradi huo na kuondoa vikwazo vyote vinavyoweza kujitokeza.

Anasema wakulima wana jukumu la kushiriki kwenye mafunzo ili waboresha chumvi wanayozalisha, wakielewa ujenzi wa kiwanda hicho unategemea ushirikiano wao katika mbinu mpya za uzalishaji.

CHANGAMOTO/ SHERIA

Inaangaliwa kitaalamu, kuna changamoto zinazoweza kujitokeza katika utekelezaji wake, ikiwamo kufikia viwango bora vya kimataifa sokoni.

Kuna mtazamo katika namna upatikanaji wa rasilimali zinazokidhi mahitaji kuendesha kiwanda hicho katika viwango vinavyohitajika, pamoja na kusimamia vizuri ushirikiano kati ya wakulima, serikali na wawekezaji.

Ujenzi wa kiwanda hiki unaendana na sheria, pia kanuni zinazolenga kulinda na kuimarisha sekta ya uzalishaji chumvi nchini, ikiwamo Sheria ya Madini, inayomamia rasilimali za madini, ikiwamo chumvi. 

Sheria hiyo inaweka taratibu za upatikanaji wa leseni za uchimbaji na uzalishaji wa madini, pamoja na masharti ya mazingira yanayohitajika katika shughuli hizo.

Aidha, Sheria ya Mazingira ya Mwaka 2004, inalenga kulinda mazingira katika shughuli za uzalishaji wa madini, hivyo kiwanda tarajiwa kiangukia katika kufuata masharti yaliyowekwa katika sheria hiyo, kuhakikisha uzalishaji chumvi hauharibu mazingira ya eneo hilo.

Sheria ya Utafiti na Maendeleo ya Viwanda nchini Tanzania ya Mwaka 2009, inalenga kuimarisha shughuli za utafiti na maendeleo katika sekta ya viwanda, ili kuchangia katika maendeleo ya uchumi kitaifa.

Hapo inasimamia masuala kama vile utafiti wa kiteknolojia, ushirikiano kati ya sekta ya umma na binafsi na uwekezaji katika maendeleo ya viwanda. Ni sheria inayosaidia kuweka mazingira mazuri kwa uvumbuzi na matumizi ya teknolojia mpya katika uzalishaji wa viwanda.