Waziri Mkuya aeleza umuhimu mfuko TIMIZA

By Rahma Suleiman , Nipashe
Published at 07:16 AM Jun 15 2024
WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Rais, Fedha na Mipango, Dk. Saada Mkuya Salum.
Picha: Mpigapicha Wetu
WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Rais, Fedha na Mipango, Dk. Saada Mkuya Salum.

WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Rais, Fedha na Mipango, Dk. Saada Mkuya Salum, amesema Mfuko wa Uwekezaji wa Pamoja (TIMIZA FUND) utaisaidia serikali kuwashirikisha wananchi wake katika uwekezaji na shughuli za kiuchumi kwa lengo la kuboresha kipato cha kuendesha maisha yao.

Aliyasema hayo jana katika hotuba yake iliyosomwa na Naibu Waziri wake, Juma Makungu wakati wa uzinduzi wa mfuko huo hafla iliyofanyika visiwani hapa.

Alisema mfuko huo utatoa fursa kwa wananchi wa kipato cha chini kushiriki katika uchumi na kuongeza kiwango cha utumiaji wa fedha na uchumi jumuishi.

Mkuya alisema uongozi wa TIMIZA FUND na wadau wanapaswa kuyafanyia kazi mambo yote waliyoahidi katika waraka wa toleo la mfuko huo ili kuendelea kujenga imani kwa wananachi.

“Usimamizi wenye weledi na uadilifu wa TIMIZA FUND unategemewa katika  kuleta maendeleo makubwa zaidi, hivyo sote tunaojihusisha na sekta hii, twendeni tukayafanye tunayoyasema kwa mujibu wa sheria na kanunui zinazotuongoza”alisema Makungu.

Naye Mkurugenzi Mkuu wa Zan Securties, Raphael Masumbuko, alisema mfuko wa uwekezaji wa pamoja utasaidia kufungua milango ya fursa mbalimbali hata zile zilizopo nje ya uwezo wa mtu mmoja mmoja na uwekezaji huo ni kwa watu wote wa vipato vya aina zote.

Mwenyekiti wa Bodi ya Zan Security, Abdulsalaam Issa Khatib, alisema mfuko huo ni chachu ya kuleta mabadiliko ya tamaduni na hamasa za wawekezaji kuweka akiba ili kuleta ushindani wa mifuko na kuleta tija kwa mifuko na Taifa kwa ujumla.

Aidha, alisema jambo hilo ni la kihistoria katika sekta ya uwekezaji kutokana na umuhimu wa masoko na mitaji ya Zanzibar na kuitaka Serikali kushauri taasisi za umma kuwekeza katika sekta ya mitaji na kujiorodhesha katika soko la hisa ili kutoa hamasa kwa mifuko ya uwekezaji.

Akizungumza kwa niaba ya Mtendaji Mkuu wa Soko la Hisa la Dar es Salaam, Emanuel Nyalali ameishukuru serikali kwa kuanzisha sera na kanuni zinazowezesha sekta za masoko na mitaji kukuwa nchini.

Aliwataka wafanyakazi kuwekeza katika mfuko huo ili kutimiza malengo waliyojipangia ikiwamo kuwekeza kwa ajili ya mahitaji ya elimu, ujenzi,ukarabati wa  nyumba, kustaafu,, gharama za safari za likizo, pamoja na  huduma za afya.

Mfuko wa uwekezaji wa pamoja umeanzishwa mwaka 2019 chini ya Zan Securties kwa lengo la kuwashirikisha wananchi  kujiunga na mfumo  wa masoko ya mitaji na dhamana ili kunufaika kiuchumi.