Wanaotorosha tumbaku kufunguliwa kesi ya uhujumu uchumi

By Halima Ikunji , Nipashe
Published at 07:56 PM Apr 02 2024
Zao la tumbaku.
MAKTABA
Zao la tumbaku.

SERIKALI imesema kiongozi yoyote atakayebainika anajihusisha na utoroshaji na ulanguzi wa tumbaku atakufunguliwa kesi ya uhujumu uchumi.

Hayo yalielezwa na Mkuu wa Wilaya ya Uyui, Zakaria Mwansasu wakati wa ufunguzi wa mkutano mkuu wa 31 wa Chama Kikuu cha Ushirika cha WETCU mkoani hapa.

Alisema utoroshaji na ulanguzi huo unadhoofisha vyama vya msingi vya ushirika na kusababisha kufa kutokana na kudaiwa fedha nyingi na taasisi za fedha.

“Napenda kutumia fursa hii kuwaonya wale wanaohusika na utoroshaji na ulanguzi wa tumbaku kuacha mara moja kwani tumepanga kuimarisha ulinzi na watakaobainika watachukuliwa hatua za kisheria.  Vitendo hivi vinaweza kukoma iwapo kila kiongozi na mwanachama watakuwa waadilifu kwa kufichua uozo huo" alisema Mwansasu.

Alisema kuwa tatizo ilo limechangia baadhi ya wakulima kukosa malipo yanayotokana na mauzo ya tumbaku, hivyo ni jukumu la viongozi wa vyama vya msingi vya ushirika kuwa wasimamizi wazuri na kufanya shughuli mbalimbali kwa uadilifu mkubwa, ili kupunguza malalamiko kwa wanachama.

Alisema endapo hali hiyo itajitokeza kwenye chama chochote msimu huu au wowote hatua kali za kisheria zitachukuliwa ili kukomesha mchezo huo mchafu katika zao la hilo.

Awali Mwenyekiti wa WETCU, Hamza Kitunga alisema mwaka huu chama hicho kupitia wanachama wake wanatarajia kupata kilo milioni 47 za tumbaku licha ya kuwepo na majanga yatokanayo na mvua za masika.