Wafanyabiashara Kabanga walalamika kubaguliwa

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 12:00 PM Jul 22 2024
Matunda.
Picha: Mtandao
Matunda.

BAADHI ya wafanyabiashara wa mazao, matunda na bidhaa za viwandani katika mpaka wa Tanzania na Burundi, Kabanga wameiomba serikali kuhakikisha wanaweka usawa kwa wazawa katika fursa za kibiashara sambamba na kutatua kero wanazokabiliana nazo mpakani hapo.

Walitoa ombi hilo juzi katika kikao cha wafanyabiashara kutoka maeneo mbalimbali ya wilaya hiyo kilichoandaliwa na kamati ya kitaifa ya uwezeshaji biashara katika forodha ya mpaka wa Kabanga kikilenga kutafuta ufumbuzi wa matatizo na kusaidia wafanyabiashara kufanya kazi katika mazingira rafiki. 

Mmoja wa wafanyabiashara hao, Christina George, alibainisha kero wanazokabiliana nazo kuwa ni pamoja na raia wa Burundi kupewa  sehemu kubwa ya ajira na uingizaji wa biashara mbalimbali nchini,  ambapo wazawa  wamekuwa walikutana na vikwazo vya kisheria wanapoingiza hitaji kupeleka bidhaa Burundi.

Alisema, kama wafanyabiashara wanahitaji kupewa fursa sawa kama wanazozipata wenzao kutoka Burundi za kuingiza bidhaa nchini bila vikwazo na wao waweze kutoa nje bila vikwazo vya aina zozote. 

Mfanyabiashara wa nafaka, John Ibrahim alisema, uingiaji wa wafanyabiashara wa nje ya nchi bila kufuata taratibu za vibali vya ununuzi wa bidhaa, unakwamisha maendeleo ya wafanyabiashara ambao na wao wanafanya shughuli ya usafirishaji nje ya nchi kwa utaratibu maalumu.

Mwenyekiti wa Soko la Kabanga, Samweli George, alisema, wafanyabiashara wa ndani wanapofungua viwanda vya uzalishaji bidhaa hujikuta wanafunga kutokana na kukosa wateja wa kununua kutokana na bidhaa zinazotoka Burundi kuingia nchini kuteka soko.

George alisema, hali hiyo inaleta mdororo kwa wazalishaji wa ndani ambao huzalisha bidhaa zinazofanana na zile zinazoingizwa na wafanyabiashara wa Burundi kwa njia za panya na kupewa vibali au kuwatumia mawakala wa ndani.

Kamshina wa Forodha kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Juma Hassan alisema, tayari wamepokea malalamiko hayo na wanayatafutia ufumbuzi ili kuhakikisha kila mfanyabiashara anafuata sheria.

Aidha, alisema kuwa ni wazi kuwa bidhaa zinazoingia bila ya kufuata utaratibu za forodha zinaathiri biashara kwa wafanyabiashara wa ndani, hivyo kamati ya kitaifa ya uwezeshaji biashara italifikisha katika vyombo vya uamuzi.