Viwanda kipaumbele Dira Maendeleo 2050

By Joseph Mwendapole , Nipashe
Published at 09:38 AM Jul 25 2024
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Mipango na Uwekezaji), Prof. Kitila Mkumbo.
Picha: Mpigapicha Wetu
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Mipango na Uwekezaji), Prof. Kitila Mkumbo.

SERIKALI imesema katika maandalizi ya Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050, imeweka kipaumbele kikubwa kwenye sekta ya viwanda lengo kubwa likiwa kuondoa utegemezi wa kununua bidhaa nyingi nje ya nchi.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Mipango na Uwekezaji), Prof. Kitila Mkumbo, alisema hayo juzi wakati akizungumza kwenye mkutano wa wadau wa viwanda.

Mkutano huo ulioandaliwa na Shirikisho la Wenye Viwanda (CTI), pia ulizindua tuzo za Rais za Mzalishaji Bora Viwandani (PMAYA) ambazo hufanyika kila mwaka kwa wenye viwanda.

Prof. Mkumbo alisema wasomi mbalimbali wamesema kwenye maandiko yao kuwa tofauti kubwa baina ya nchi zilizoendelea na zinazoendelea zinatokana na  maendeleo katika sekta ya viwanda. Alisema nchi zilizoendelea kwamba nchi tajiri zina viwanda vingi wakati nchi zinazoendelea hazina viwanda na zinategemea kuagiza bidhaa nje ya nchi.

“Itakuwa vigumu sana kutengeneza Dira ya Taifa bila kuweka viwanda katikati ya dira hiyo kwa sababu hilo ni la msingi na tafiti nyingi zinaonyesha kuwa hatuwezi kuendelea kwa kuendelea kununua bidhaa nje ya nchi. Lazima  tuwe na viwanda vingi tuuze  nje,” alisema.

Alisema katika utafiti ambao umefanywa na serikali katika maandalizi ya dira hiyo uliohusisha watu 7,668 nchi nzima, waliochaguliwa kisayansi walitaka vipaumbele vitano viwapo kwenye dira hiyo.

Waziri Mkumbo alitaja moja ya vipaumbele vilivyotajwa na wananchi hao kuwa ni viwanda na kwamba asilimia 65 ya malighafi zinazotumika viwandani zinatokana na kilimo, hivyo kilimo nacho kitaendelea kuwa kipaumbele kwenye dira hiyo.

Alisema kipaumbele kingine kilichotajwa kwenye utafiti huo ni uwekezaji mkubwa kwenye rasilimali watu kwa kuwa uchumi wa viwanda unahitaji watu walioelimika vyema katika taaluma mbalimbali.

“Lazima dira yetu ituelekeze kuwekeza kwenye elimu na si elimu tu bali elimu iliyo bora,” alisema Prof. Mkumbo.

Mkurugenzi Mtendaji wa CTI, Leodegar Tenga, alisema wadau wa viwanda wamekutana kujadili Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050 na kuzungumzia maendeleo ya viwanda kwa ujumla ili kuhakikisha maendeleo ya sekta hiyo hayasahauliki kwenye dira hiyo.

“Tunashukuru Waziri amezungumza kwamba bila viwanda hakuna maendeleo na ametoa mifano ya nchi nyingi zilizoendelea zilivyopiga hatua kwenye viwanda.

“Hakuna nchi duniani hata moja ambayo iliwahi kupiga hatua kubwa kiuchumi bila kuwekeza kwenye viwanda, hivyo lazima tuwe na mikakati madhubuti. Kuna msemo wa Kiswahili kwamba kupanga ni kuchagua, hivyo tuchague kuwekeza kwenye viwanda ili tusonge mbele,” alisema.

Aidha, alisema ili viwanda vifanye kazi vizuri lazima serikali iwekeze pia kwenye ujenzi wa miundombinu ya barabara na reli na kwenye rasilimali watu.

“Maono ya nchi ni kujipanga ili tutimize tulichopanga kwa hiyo CTI tunaamini viwanda ni muhimu na ili kupata rasilimali lazima tuwe na kilimo kwa hiyo lazima tuwekeze pia kwenye kilimo.

“Tumefungua masoko mengi upande wa Afrika Mashariki (EAC),  kusini mwa jangwa la sahara (SADC) sasa tujipange kuuza bidhaa zetu za viwanda nje ya nchi badala ya sisi kuwa soko la bidhaa za wenzetu,” alisema Tenga.

Mwenyekiti wa CTI, Paul Makanza, alisema Tanzania inapaswa kuwa na viwezeshaji vinavyofaa kama teknolojia, rasilimali watu na miundombinu.

“Zaidi ya hayo, ni lazima tujenge msingi imara wa amani, utulivu, umoja, kujitegemea, na muundo wa utawala unaounga mkono uwajibikaji, uwazi na kufanya maamuzi shirikishi.

“Lazima tutafakari kuhusu maisha yetu ya zamani, tuelewe maisha yetu ya sasa, na kwa ujasiri kuunda maisha yetu ya baadaye na tunahitaji maono wazi yanayoungwa mkono na chaguzi za kimkakati na inayoungwa mkono na maadili,” alisema.