TIRA yataka weledi huduma za bima

By Allan Isack , Nipashe
Published at 07:24 AM Jul 27 2024
Kamishna wa Bima Tanzania, Dk. Baghayo Saqware.
Picha: Mtandao
Kamishna wa Bima Tanzania, Dk. Baghayo Saqware.

MAMLAKA ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA), imewataka wadau wa sekta hiyo nchini, kufanya shughuli ya utoaji wa huduma za bima kwa kuzingatia weledi, badala ya kufanya udanganyifu.

Kamishna wa Bima Tanzania, Dk. Baghayo Saqware, alisema hayo jana katika taarifa aliyoitoa jijini Arusha, wakati akifungua mkutano wa nane wa Chama cha Washauri Bima Tanzania (TIBA).

Alisema endapo itabainika kuwa wapo watoa huduma wamekiuka kanuni, utaratibu na miongozo ikiwamo kufanya udanganyifu watachukuliwa hatua kali za kisheria.

“Ninasisitiza mfanye biashara ya bima kwa ueledi na kuepuka udanganyifu huku mkifuata sheria na miongozo inayotolewa na mamlaka,” alisema Dk. Saqware.

Aidha, aliwataka wadau hao kuendelea kutoa elimu sahihi ya bima kwa wananchi, kuwashawishi kutumia bidhaa za huduma za bima za kujikinga na majanga ya mali, afya, biashara na kilimo.

Alisema TIRA inatambua mchango wa wadau hao katika kuendeleza soko la bima hapa nchini na ili kuhakikisha soko linakuwa salama wameweka mazingira mazuri ya sheria, kanuni na miongozo.

“Serikali imetengeneza taswira chanya katika soko la bima ili kumlinda mtoa huduma na mtumiaji kwa kufanya hivyo imetuheshimisha na imetusaidia kupata mafanikio makubwa,” alisema Dk. Saqware.

Katika mkutano huo, Rais wa TIBA, Okoth Oloo, alisema washiriki wa mkutano huo, wametoa maeneo mbalimbali hapa nchini na baadhi ya nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC)  zikiwamo Uganda,Kenya,Rwanda na Burundi.

Aidha, alisema watajadiliana namna sheria na usimamizi katika sekta ya bima kama inakuza soko au kuchochea soko hilo kukua.

Alisema chama hicho kwa kushirikiana na serikali wataendelea kusimamia ueledi, uadilifu na uaminifu kwa watoaji wa huduma za bima.

Mwenyekiti wa maandalizi ya mkutano wa TIBA, Anna Lema, alisema utafanyika kwa siku tano utajumuisha washiriki zaidi ya 250 wakiwamo kutoka nchi wanachama wa EAC.

“Tunatarajia washiriki watajifunza na kuelewa mambo yote watakayokuwa wamefundishwa kwenye mada mbalimbali zitakazotolewa na watoa mada wetu,” alisema.