TCRA yajivunia TEHAMA katika ukuaji wa uchumi

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 09:56 AM Jul 25 2024
Ukuaji wa uchumi.
Picha mtangdao
Ukuaji wa uchumi.

MAMLAKA ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), imesema uchumi wa Tanzania umekua kwa kasi kubwa katika kipindi cha miaka mitatu kutokana na kukua kwa matumizi ya teknolojia ya habari na mawasiliano (TEHAMA) katika maeneo mengi.

Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TCRA ambaye ni Mkurugenzi wa Masuala ya Kisekta,  Mhandisi Mwesigwa Felician, aliyasema hayo jana wakati akizungumza na maofisa wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi Tanzania (JWTZ) waliotembelea ofisi kuu za TCRA, Dar es Salaam, ikiwa ni ziara ya mafunzo kuhusu masuala ya usalama mtandaoni.

Maofisa waliotembelea mamlaka hiyo wanahudhuria mafunzo hayo ni maofisa wanafunzi wa Chuo cha Ulinzi na Intelijensia Tanzania (TDIC) walioko kwenye wiki ya mwisho ya mafunzo ya wiki 10 ya masuala mbalimbali ya kijeshi.

Kati yao walikuwa wakufunzi wanane (8) na maofisa 31, sita wanawake.

Alisema TEHAMA imechangia maendeleo ya sekta mbalimbali zikiwamo elimu, afya, ulinzi na uchumi wa nchi.

Aidha, alitoa mifano wa namna TEHAMA ilivyowezeshi kwenye huduma za kifedha na miamala ya simu, matumizi ya pesa mtandao kwa benki, na ukuaji wa uchumi kidijitali.

“Akaunti za pesa kwa simu zimeongezeka kwa karibu mara mbili ndani ya miaka mitano, huku kukiwa na ukuaji wa asilimia tano kati ya Aprili na Juni mwaka huu.

Takwimu za hali ya mawasiliano robo mwaka ya Aprili-Juni 2024 iliyotolewa na TCRA inaonesha kuwa akaunti za pesa kwa simu ziliongezeka kutoka 25,864,318 mwaka 2019 hadi 52,875,129 mwaka 2023 na kufikia 55,523,067 Juni, mwaka huu.

Alisema akaunti hizo zilifanya miamala 5,273,086,154 Juni, mwaka huu, ikilinganishwa na miamala 3,021,142,958 mwaka 2019.

Ujumbe huo uliongozwa na Brigedia Jenerali Salum Mnumbe, Mkuu wa Chuo cha Ulinzi na Intelijensia Tanzania.

Maofisa hao walitembelea kitengo cha Mwitikio wa Majanga ya kompyuta (TZ-CERT), kitengo cha usimamizi wa mifumo ya mawasiliano na makumbusho ya mawasiliano.

Maofisa wanafunzi wa JWTZ-TDIC wakipata maelezo kwenye Makumbusho ya Mawasiliano TCRA walipokuwa kwenye ziara ya Mafunzo kwenye ofisi hizo.

Washiriki walisema wamejifunza na kujionea namna TCRA inavyofanya kazi kwa ufanisi uliorahisishwa kwa uwepo wa mifumo ya kompyuta inayowasiliana hivyo kuharakisha na kurahisisha utoaji wa huduma hususani leseni za huduma za mawasiliano.

Brigedia Jenerali Mnumbe aliishukuru TCRA kwa kusimamia rasilimali za masafa kwa ufanisi, hivyo na kuzuia mwingiliano kati ya bendi. 

“Hali hii imeboresha usalama na mawasiliano, hasa kwa vyombo vya usalama ikiwamo JWTZ,” alisema.

Pia alipongeza mipango ya TCRA au utoaji elimu ya namna ya kuripoti matukio ya utapeli, ulaghai na kihalifu mtandaoni kwa kutumia namba 15040, na kwamba elimu hiyo imechangia kupunguza matukio ya uhalifu mtandaoni.

Mkufunzi mwelekezi wa masomo ya usalama mtandaoni wa chuo hicho, Meja Erick Nyiti, alisema wamejifunza na kujionea mengi na makubwa katika ziara hiyo. 

“Hii inatupa chachu sisi kuongeza ujuzi kwenye eneo la TEHAMA,” alisema.

Akihitimisha mafunzo hayo, Mhandisi Mwesigwa aliwaomba maofisa hao kuzidisha weledi kwenye kazi na kuzidi kujifunza zaidi masuala mbalimbali ya TEHAMA.

Aliongeza kuwa ulimwengu unabadilika kwa kasi, na kwa matumizi ya teknolojia ya akili mnemba (AI) yanaongezeka, jambo linaloongeza tishio kwenye anga la kidijitali.

“Kwa sasa matumizi ya akili mnemba yameshamiri hivyo hatari ya uhalifu mtandaoni inaongezeka inabidi nasi tuwe tayari kupambana,” alisema.

Kiongozi huyo wa TCRA alieleza kufurahishwa kwake kwa uhusiano mzuri baini ya mamlaka hiyo na Jeshi la Wananchi wa Tanzania.