Serikali yazindua matumizi sahihi ya mbolea kwa wakulima

By Gideon Mwakanosya , Nipashe
Published at 08:31 PM Jul 25 2024
Baadhi ya watendaji wa sekta ya kilimo kutoka mkoa wa Ruvuma na Mamlaka ya udhibiti wa ubora wa mbolea Tanzania(TFRA)wakimsikiliza Naibu Waziri wa Nishati Judith Kapinga(hayupo pichani)wakati wa usinduzi wa kampeni ya Uhamasishaji wa matumizi ya mbolea.
Picha: Gideon Mwakanosya
Baadhi ya watendaji wa sekta ya kilimo kutoka mkoa wa Ruvuma na Mamlaka ya udhibiti wa ubora wa mbolea Tanzania(TFRA)wakimsikiliza Naibu Waziri wa Nishati Judith Kapinga(hayupo pichani)wakati wa usinduzi wa kampeni ya Uhamasishaji wa matumizi ya mbolea.

MATUMIZI ya mbolea nchini,yameongezeka kutoka wastani wa tani 363,599 katika msimu wa kilimo 2021/2022 hadi kufikia tani 840,714 kwa msimu wa kilimo 2023/2024.

Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania, Joel Lauren amesema hayo wakati wa uzinduzi wa kampeni ya kuhamasisha usajili wa wakulima na matumizi sahihi ya mbolea uliofanyika wilayani Mbinga.

Amesema,Mkoa wa Ruvuma ambao ni kati ya mikoa ya kimkakati ya uzalishaji wa chakula hapa nchini, kwa miaka ya karibuni umeongoza kwa matumizi ya mbolea ambapo msimu 2022/2023 Mkoa huo ulitumia  zaidi ya tani 83,472.

"Katika msimu 2023/2024 Mkoa wa Ruvuma umetumia tani 100,000,hivyo kuendelea kuwa kinara kwa matumizi ya mbolea na kuwa miongoni mwa Mikoa tegemezi katika uzalishaji wa chakula hapa nchini"amesema.

Laurent alitaja mikoa inayofuatia kwa matumizi ya mbolea ni Njombe tani 75,358,Mbeya tani 75,252,Songwe tani 71,230 na Mkoa wa Iringa ambao umetumia tani 44,214.

Amesema,matumizi ya mbolea kwa sasa ni muhimu kutokana na kuongezeka kwa idadi ya watu kunakohitaji ongezeko la uzalishaji wa chakula ili kukidhi mahitaji,ukuaji wa miji,miundombinu na huduma za kijamii zinazochangia kupunguza eneo linalofaa kwa kilimo.

Ameeleza kuwa,matumizi sahihi ya mbolea kunaongeza tija na kuchangia kukuza kipato cha mkulima mmoja mmoja,ukuaji wa sekta ya kilimo na pato la Taifa kwa ujumla.

Ameongeza kuwa,hapa nchini kuna mbolea za viwandani na mbolea za asili ambazo zinatumiwa na wakulima,lakini changamoto ni matumizi kidogo ya mbolea kwa baadhi ya maeneo kunatokana na dhana potofu kwamba mbolea inaharibu ardhi na baadhi ya wakulima kukosa elimu ya matumizi sahihi ya mbolea”alisema Laurent.

Amewakumbusha wakulima umuhimu wa kutumia mbolea katika uzalishaji wa mazao kwenye mashamba yao kwani unasaidia  kurutubisha,kuboresha afya ya udongo na kuzalisha mazao kwa wingi katika eneo dogo.

Kwa upande wake  Naibu Waziri wa Nishati Judith Kapinga alisema,sekta ya kilimo ndiyo mhimili wa uchumi wa Tanzania na inaajiri takribani theluthi mbili ya nguvu kazi ya Taifa na inachangia asilimia 65 ya malighafi za viwandani,asilimia 100 ya usalama wa chakula na zaidi ya asilimia 26 ya Pato la Taifa.

Kapinga alisema,katika mazingira ambayo kilimo ndiyo  sekta ya uchumi,maendeleo ya mwananchi na Taifa kwa ujumla yanategemea zaidi ufanisi katika sekta hiyo.

Alisema,serikali ya awamu ya sita imedhamiria kufanya mapinduzi  makubwa katika sekta ya kilimo kwa kuongeza bajeti ya wizara kutoka takribani Sh.bilioni 294 mwaka 2021/2022 hadi kufikia  Sh.trilioni 1.24 kwa mwaka 2024/2025.

Amewataka wakulima hapa nchini wakiwemo wa wilaya ya Mbinga na Mkoa wa Ruvuma,kuchangamkia fursa zinazotolewa na Serikali kwa kujisajili katika mfumo wa kidijitali kupitia Ofisi za Watendaji wa vijiji na mitaa.

Naibu Waziri Kapinga alisema,kujisajili kwenye mfumo wa kidijitali kutawaweza wakulima kununua mbolea kwa gharama nafuu,kuongeza uzalishaji,kuboresha maisha yao na kuchangia ukuaji wa uchumi.

Ametaja faida nyingne kwa wakulima kujisajili  kwenye mfumo wa kidijitali,ni kuiwezesha serikali kupata takwimu sahihi zitakazotumika kuweka mipango ya kuwaendeleza wakulima,sekta ya kilimo na kupata huduma za ugani,taarifa za masoko na huduma za kifedha kupitia kanzidata.

Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Ruvuma Jumanne Mankhoo,ameipongeza mamlaka ya udhibiti wa ubora wa mbolea kwa kusimamia vema upatikanaji wa pembejeo za Ruzuku iliyosaidia kupatikana kwa wingi na kwa urahisi katika meneo mengi ya Mkoa huo.

Naye Mkurugenzi wa uzalishaji wa ndani na ununuzi wa mbolea kwa pamoja wa TFRA Dk. Louis Kasera alisema,kampeni hiyo inalenga kuhamasisha wakulima kote nchini juu ya matumizi sahihi ya mbolea ili waweze kongeza uzalishaji.

Amewahakikisha wakulima kuwa,mpango wa mbolea za ruzuku utaendelea kutolewa hadi katika msimu wa kilimo 2024/2025 na kuwataka wakulima waongeze juhudi na kutumia mbolea kwenye shughuli zao za kilimo.