Serikali yatoa bil.3/- utekelezaji mradi wa umwagiliaji Iramba

By Thobias Mwanakatwe , Nipashe
Published at 08:15 PM Apr 02 2024
Mkuu wa Wilaya ya Iramba, Suleiman Mwenda.
THOBIAS MWANAKATWE
Mkuu wa Wilaya ya Iramba, Suleiman Mwenda.

SERIKALI imeipatia Wilaya ya Iramba mkoani Singida Sh.bilioni tatu kwa ajili ya utekelezaji wa mradi wa umwagiliaji mashamba uliopo katika Bonde la Wembere.

Katika mradi huo zaidi ya hekari 36,000, zimetengwa kwa ajili ya kilimo cha umwagiliaji.

Mkuu wa Wilaya ya Iramba, Suleiman Mwenda, aliyasema hayo wakati akizungumza na wananchi wa Kata ya Urughu kwenye mkutano wa hadhara wa mbunge wa Iramba Magharibi, Dk. Mwigulu Nchemba. 

Mwenda alisema utekelezaji huo ni agizo lililotolewa na Rais Samia Suluhu Hassan la kutaka yachaguliwe maeneo ya kuanzisha kilimo cha umwagiliaji ili kuhakikisha usalama wa chakula na kilimo.

"Mradi huu utakapokamilika utawafanya wananchi walime wakati wote wa kiangazi na masika kwa sababu watakua wana uwezo wa kuhifadhi maji, tayari wataalam na maofisa wa umwagiliaji wameshafika kujitambulisha ofisini kwangu," alisema.

Dk. Nchemba ambaye pia ni Waziri wa Fedha, aliwaomba wananchi kuendelea kumuunga mkono Rais Samia Suluhu Hassan kwa sababu anaendelea kufanya makubwa yanayoboresha ustawi na kujali afya zao.

Alisema fedha zinazoletwa Wilaya ya Iramba na maeneo mengine nchini zinakwenda kujenga miradi mbalimbali ya maendeleo, vikiwemo vituo vya afya katika kila tarafa na maeneo muhimu.

"Anajali afya yako anakupa mtaji wa kufanya kazi kwa sababu anaweza kuwa na mipango mizuri ya kazi lakini asipokua na afya njema hawezi kuitekeleza mipango hiyo," alisema.

Aliongeza kuwa: "Mama ametafsiri kwa vitendo kauli ya kuwapenda Watanzania na anashughulikia tatizo la ugumu wa maisha kwa kupeleka miradi mikubwa ya umwagiliaji hata ngazi ya kijiji ambayo inatoa majawabu".

Dk. Mwigulu alisema anaorodha ya matatizo na kutoa majawabu kivitendo kwa sababu nchi nzima kuna miradi ya umwagiliaji na miradi ya kufungua barabara ambapo itabadilisha maisha ya Watanzania kutoka katika ugumu.