ASKOFU Mkuu Jude Thaddeus Ruwa'ichi, amesema Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Dar es Salaam litaendelea kushirikiana na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kuhamasisha watu kulipa kodi.
Amesema watafanya hivyo kwa sababu suala hilo ni nyeti kwa maendeleo ya nchi.
Ruwa’ichi alisema hayo jana wakati akizungumza na Kamishna Mkuu wa TRA, Yusuph Mwenda, alipotembelewa nyumbani kwake, jijini Dar es Salaam.
Mwenda alimtembelea Askofu Ruwa’ichi ikiwa ni mwendelezo wa kuwashukuru walipakodi.
Askofu Mkuu Ruwa'ichi alisema suala la kulipa na kukusanya kodi linalohusu maendeleo ya nchi na ni sehemu ya wajibu wa kiraia.
Pia alifurahishwa na mfumo wa ukusanyaji wa kodi unaofanywa sasa na ukaribu ulioko baina ya TRA na wananchi.
"Kwa niaba ya Watanzania wenzangu, niwapongeze kwa kazi kubwa mnayoifanya. Niwahakikishie kwamba kadri ya nafasi na uwezo wetu, tutajitahidi kuwahimiza watu wazingatie na waenzi wajibu wa kulipa kodi kwa ajili ya maendeleo yao wenyewe.
"Ninafurahi kwa msisitizo ulioweka kwamba, katika kukusanya kodi hambagui huyu wala yule, mnatafuta kuwatendea wote haki, ninaomba hilo lidumishwe na litiliwe mkazo," alisema.
Askofu Mkuu Ruwa'ichi alisema TRA inafanya vizuri inapolenga kila raia kulipa kodi inayoendana na uwezo wa mtu husika na fedha hizo kutumika kwa ajili ya watu wote kuleta maendeleo bila kujali itikadi zao.
Kamishna Mkuu Mwenda alisema lengo la kumtembelea Askofu Ruwa'ichi ni kumshukuru kwa mchango wake katika kuhamasisha ulipaji wa kodi.
Mwenda alisema Desemba ni mwezi wa kuwashukuru walipakodi na kuzitaja baadhi ya taasisi zilizoko chini ya Kanisa Katoliki ambazo zimekuwa na mchango katika kodi.
Alizitaja taasisi hizo kuwa ni sekta za elimu na afya ambapo wakati mwingine wamekuwa wakisamehewa kodi kulingana na sheria za Kodi.
Mwenda alisema kulipa kodi kwa maslahi ya nchi ni jambo la kiimani kwa sababu zinapokusanywa huelekezwa katika shughuli za maendeleo zikiwamo elimu, afya na miundombinu.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED