NEMC yatoa cheti cha Tathmini ya Mazingira miradi 9,000

By Joseph Mwendapole , Nipashe
Published at 10:00 AM Jul 23 2024
Waziri wa Viwanda na Biashara, Selemani Jafo.
Picha: Mtandao
Waziri wa Viwanda na Biashara, Selemani Jafo.

BARAZA la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), limetoa Cheti cha Tathmini ya Mazingira (EIA), kwenye miradi 9,000 yenye thamani ya Sh. trilioni 40 ndani ya kipindi cha miaka mitatu.

Hayo yalisemwa jana jijini Dar es Salaam na Waziri wa Viwanda na Biashara, Selemani Jafo, wakati akizungumza na uongozi na wafanyakazi wa baraza hilo alipokwenda kuwaaga Mikocheni baada ya kuteuliwa kwenye nafasi mpya.

Alisema moja ya mafanikio makubwa anayojivunia ni baraza hilo kutoka kwenye utoaji wa huduma katika mfumo wa analojia na kwenda kidijitali ambako kumerahisisha utoaji wa huduma kwa haraka na kwa ufanisi mkubwa.

Alisema zamani alikuwa akitia saini vyeti vya EIA kwa mfumo wa analojia, lakini baada ya mageuzi makubwa sasa vinatolewa kidijitali hali ambayo imeondoa usumbufu kwa wawekezaji wanaofika kwenye baraza hilo. 

“Zamani cheti cha EIA kilikuwa kinazunguka sana, lakini leo hii waziri akishasaini tu kinakuwa tayari kwa ajili ya kuchapishwa na mwekezaji anapata ndani ya muda mfupi kwa hili nawapongeza sana na endeleeni kuboresha mifumo dunia inakwenda kidijitali,” alisema.

“Tumefanikisha uwekezaji wa karibu miradi 9,000 wenye thamani ya trilioni 40 sio jambo dogo, mnafanyakazi kubwa sana mmesaidia sana na ukiangalia NEMC imebadilika sana sio ile ambayo ilikuwa inalalamikiwa kila wakati,” alisema.

Aidha, Jafo alisema NEMC imesaidia kuhamasisha wananchi kufahamu umuhimu wa miti na kwa sasa vijana wengi wamejiajiri katika biashara ya kuuza mbegu za miti kwenye maeneo mbalimbali nchini.

Alisema akiwa kwenye wizara ya mazingira, alifanikiwa kushirikiana na baraza hilo kupambana na uchafuzi wa mazingira ikiwamo kukomesha utiririshaji wa maji taka unaofanywa na baadhi ya viwanda.

“Tumefanya pamoja kama timu na kwa kuheshimiana ndio sababu tumefika hapa tulipo na naomba mafanikio haya yalindwe kuhakikisha mazingira yanatunzwa na turithishe vizazi vijavyo mazingira bora,” alisema.

Aliutaka uongozi wa NEMC kuwawekea mazingira mazuri wafanyakazi ili wawe na motisha wa kufanyakazi akisema kuwa mtu mwenye msongo wa mawazo hawezi kufanyakazi kwa ufanisi.

“Msiwadharau madereva, wahudumu wa ofisi kwasababu wote hatuwezi kuwa wakurugenzi lazima ofisi iwe na watumishi wa kada mbalimbali kwa hiyo mdogo amheshimu mkubwa na mkubwa amheshimu mdogo pia,” alisema Jafo.

“Ukiwa kwenye nafasi ya uongozi usiwaumize wenzako kwa sababu huwezi kujua huyu ambaye unamdharau kesho atakuwa nani, ishi kwa nidhamu na kuheshimu kila mtu kama akiba yako itakayokusaidia siku za baadaye,” alisema Waziri Jafo.

Alisema wanapaswa kusimamia kikamilifu sheria, taratibu na kanuni ili kuiweka nchi kwenye mazingira mazuri na kuwasaidia wawekezaji kufanya shughuli zao bila kusubiri kwa muda mrefu kupata huduma wanazotaka.

Mkurugenzi Mkuu wa (NEMC), Dk. Immaculate Semesi, alisema kwa muda waliokuwa pamoja NEMC imefanikisha kusimamia uzingatiaji wa mazingira na walifanya kaguzi 3,000 za mazingira kwenye maeneo mbalimbali nchini.

“Tumeendelea kusimamia zuio la matumizi ya mifuko ya plastiki iliyopigwa marufuku ambapo zaidi ya tani 90 ilikamatwa na kutaifishwa na kuzuia utupaji ovyo wa taka hatarishi na vibali zaidi ya 1,000 vya usafirishaji wa taka hizo vilitolewa na baraza,” alisema.

Aidha, alisema NEMC ilipokea malalamiko kwenye jamii 5,000 na liliyatatua na katika kipindi cha miaka mitatu walifanikiwa kupiga marufuku kelele kwenye nyumba za ibada.