Mwinyi asisitiza utawala bora kwa maendeleo

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 11:40 AM Dec 19 2024
Mwinyi asisitiza utawala bora kwa maendeleo.
Picha: Mpigapicha Wetu
Mwinyi asisitiza utawala bora kwa maendeleo.

RAIS wa Zanzibar, Dk. Hussein Ali Mwinyi, amesema suala la kuimarisha utawala bora ni jambo la msingi ili kuleta maendeleo ya nchi.

Kutokana na umuhimu huo, amewasihi watumishi wa umma na sekta binafsi binafsi kuongeza juhudi, uzalendo na uadilifu katika kulitumikia taifa.

Dk. Mwinyi, kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na idara ya mawasiliano Ikulu, Zanzibar, aliyasema hayo jana katika ukumbi wa Ziwani Polisi Zanzibar kwenye maadhimisho ya Kilele cha Wiki ya Ukaguzi ya Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Zanzibar.

Alisema wajibu wa kuimarisha utawala bora hasa kwa matumizi ya rasilimali za umma, si wa serikali na ofisi ya CAG pekee bali ni kwa kila mtumishi.

Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, alisema itaendeleza juhudi za kuijengea mazingira mazuri ofisi ya CAG ili itekeleze vizuri kazi zake kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu zilizopo kitaifa na kimataifa na kwenda sambamba na mabadiliko ya mara kwa mara ya ukaguzi duniani.

Dk. Mwinyi alibainisha kuwa ofisi ya CAG imeisaidia serikali kutekeleza kwa ufanisi malengo na mipango yake. Alisema maendeleo makubwa yaliyofikiwa serikalini yanatokana na mchango wa udhibiti na ukaguzi bora wenye kuzingatia uwajibikaji, nidhamu na uwazi katika matumizi ya rasilimali za umma.

Rais Mwinyi pia alisema miongoni mwa faida zinazopatikana kwenye ofisi ya CAG ni pamoja na kusaidia kuongeza pato la serikali na CAG kupitia ripoti yake ya kila mwaka, huishauri serikali juu ya mbinu bora za kuziba mianya ya upotevu wa makusanyo ya mapato ya serikali, kuibua vyanzo vipya vya mapato na kuwapo kwa usimamizi bora wa rasilimali za umma. 

Alisema ufanisi unaotokana na utekelezaji wa kazi za ukaguzi una mchango mkubwa kwa serikali hasa kuimarisha uchumi wa Zanzibar na hadi kufikia mwaka 2023 kasi ya ukuaji wa uchumi umefikia wastani wa 7.4% ikilinganishwa na 1.3% ya mwaka 2020.

Dk. Mwinyi aliongeza kuwa mafanikio ya kazi za ukaguzi wa rasilimali za umma, yameimarisha utoaji wa huduma za jamii ikiwamo elimu, afya, majisafi na salama, nishati ya umeme na huduma zingine. 

Pia aliongeza kuwa kazi za ukaguzi wa rasilimali fedha na rasilimali zingine zimeimarisha utekelezaji wa miradi ya ujenzi wa miundombinu ya barabara, bandari, viwanja vya ndege, viwanja vya michezo na masoko.

Alibainisha kuwa mafanikio hayo yamechangiwa na udhibiti na ukaguzi bora wa rasilimali za umma na serikali hupokea na kuzifanyia kazi hoja, ushauri na mapendekezo yanayotolewa na CAG kupitia ripoti zake za kila mwaka.

Dk. Mwinyi aliahidi kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendelea kuimarisha ofisi ya CAG kwa kuendelea kufanikisha malengo na mipango ya sasa na baadaye ya ofisi hiyo kwa kadiri hali ya uchumi itakavyoruhusu.

Katika hatua nyingine, Rais Mwinyi alipongeza ushirikiano wa karibu uliopo baina ya ofisi ya CAG, serikali na Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi ya Tanzania kwa kufanikisha kazi za ukaguzi wa hesabu za serikali.

Naye Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Sheria, Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Haroun Ali Suleiman, alisema juhudi za Rais Dk. Mwinyi za kuimarisha umoja, amani na maendeleo na mshikamao kumeifanya Zanzibar kuwa nchi ya mfano kwa kasi ya maendeleo yanayowashangaza wageni kutoka mataifa mbalimbali.

Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali Zanzibar, Dk. Othman Abbas Ali, alibainisha kuwa maadhimisho hayo ni fursa adhimu kwa taasisi za umma kuwatumia wataalamu wao kuongeza uwajibikaji, kubadilishana uzoefu na kujifunza mbinu bora za kukabiliana na uhujumu wa uchumi, kuongeza uwazi na uwajibikaji.

Aliongeza kuwa kujadiliwa kwa ripoti za CAG kila mwaka katika Baraza la Wawakilishi kumeendelea kuleta tija ya usimamizi wa rasilimali na matumizi ya fedha za umma kwa taasisi mbalimbali na kujenga uelewa kwa wananchi juu ya utendaji wa ofisi hiyo.

Maadhimisho ya Wiki ya Ukaguzi ya ofisi ya CAG Zanzibar kwa mwaka 2024, yenye kauli mbiu isemayo “Kuimarika kwa Ukaguzi wa Rasilimali za Umma Kunaongeza Ufanisi na Kuleta Tija Nchini” yalianza Desemba 12, mwaka huu na kufikia kilele jana.