Moto wateketeza vibanda 10 vya wafanyabiashara

By Ida Mushi , Nipashe
Published at 10:09 AM Jul 25 2024
Moto wateketeza vibanda 10 vya wafanyabiashara.
Picha: Idda Mushi
Moto wateketeza vibanda 10 vya wafanyabiashara.

MOTO ambao chanzo chake hakijajulikana, umeteketeza vibanda 10 kati ya 60 vya wafanyabiashara wadogo kando ya Kituo cha Mabasi Msamvu, Manispaa ya Morogoro.

Mwandishi alifika eneo hilo juzi saa nne usiku na kushuhudia moto huo ukichochewa zaidi na mbao na fito zilizotumika kujenga vibanda hivyo huku askari wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji wakiwa katika harakati za kuuzima.

Baadhi ya mashuhuda wa tukio hilo, wakiwamo Mohamed Ally na Freddy Makungu, walisema moto huo ulianza saa tatu usiku.

“Tulianza jitahada za kuuzima na kutoa taarifa kwa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji ambao walifika eneo la tukio kusaidia kuudhibiti,” alisema Makungu.

Mashuhuda hao pia walidai kilichosababisha moto huo ni jiko la mkaa lililoachwa likiwaka katika moja ya vibanda hivyo. Hii si mara ya kwanza kwa tukio la moto kuripotiwa maeneo hayo.

Mwenyekiti wa Mtaa wa White House, Kata ya Mafisa, Manispaa ya Morogoro iliko stendi hiyo, Saidi Yasini Daudi, alisema kuwa hadi jana, walikuwa hawajajua hasara iliyosababishwa na moto huo.

Ofisa Operesheni kutoka Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Morogoro, Mrakibu Msaidizi, Daniel Myalla alisema wamefanikiwa kuudhibiti moto huo usiku wa kuamkia jana kwa kutumia askari na vijana wa kujitolea.

Alisema walidhibiti moto huo kabla haujaleta madhara kwa binadamu na bidhaa zaidi kwa wafanyabiashara ingawa baadhi ya mali na vibanda vimeteketea.