Jiji latuma salama kwa wazoa takataka

By Peter Mkwavila , Nipashe
Published at 07:49 AM Jul 27 2024
Jiji latuma salama kwa wazoa takataka.
Picha:Mtandao
Jiji latuma salama kwa wazoa takataka.

HALMASHAURI ya Jiji la Dodoma imesema imejipanga kuviondoa na kuviburuza mahakamani vikundi vyote vinavyojihusisha na ukusanyaji taka kwenye kata na mitaa ambavyo havina mikataba na vinaendelea kujipatia fedha.

Mkuu wa Kitengo cha Usafi na Udhibiti wa Taka Ngumu, Dickson Kimaro, alisema hayo jana baada ya kubaini kuwapo kwa vikundi vinavyojihusisha na uzoaji taka ambavyo havina mikataba na vinaendelea kuziibia kaya kwa kutoza fedha bila kutoa risiti ya mashine (POS). 

Alisema wamebaini kuwapo kwa  vikundi ndani ya mitaa na kata ambavyo mikataba yao imeisha lakini vinaendelea kuiba mapato ya jiji huku vikitambua kuwa kufanya hivyo vinawaibia watu. 

Kimaro alisema pamoja na kukosa mikataba kwa vikundi hivyo, pia vimebainika havina mashine ya kutolea risiti kwa ajili ya malipo badala yake fedha hizo zinatolewa kienyeji bila kufikishwa jiji. 

"Kwa kweli halmashauri haitakaa kimya kwa vikundi vyote vitakavyobainika kutokuwa na mashine za risiti  na mikataba ambayo hutolewa na jiji. Wakikamatwa  hatua za sheria ndogo za Halmashauri ya Jiji zitachukuliwa ikiwamo kuwaburuza mahakamani kutokana na wizi huo," alisisitiza.  

Ofisa huyo pia alivitaka vikundi  vinavyokusanya taka ambavyo vimesajiliwa na kupewa mikataba kuacha tabia ya kuzitupa kwenye maeneo yasiyo rasmi kama vile kwenye makorongo, hivyo vinatakiwa kuzipeleka sehemu iliyotengwa na halmashauri ya dampo la Chidaya. 

Kimaro pia alivitaka vikundi hivyo vinavyokusanya taka kutumia fursa hiyo kutoa elimu kwa wananchi ili waweze kushirikiana katika kuhakikisha kuliweka Jiji la Dodoma kwenye hali ya usafi kwenye mitaa na maeneo wanayoishi. 

Alisema kuwa fursa hiyo ya elimu ikitolewa Halmashauri ya Jiji itakuwa kwenye hali ya usafi wa mazingira na kila mkazi atahakikisha anajilinda mwenyewe kwa kutokutupa taka hovyo kwenye mitaa na majumbani wanakoishi watu.