CTI wataka Dira ya 2050 iweke kipaumbele kwa viwanda

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 01:34 PM Jul 23 2024
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Mipango na Uwekezaji), Prof Kitila Mkumbo (katikati) akiwa na viongozi wa Shirikisho la Wenye Viwanda (CTI),alipokwenda kufungua kongamano kuhusu dira ya taifa ya 2050 na uzinduzi wa Tuzo za Rais kwa Mzalishaji Bora Viwandani
Picha: Mpigapicha Wetu
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Mipango na Uwekezaji), Prof Kitila Mkumbo (katikati) akiwa na viongozi wa Shirikisho la Wenye Viwanda (CTI),alipokwenda kufungua kongamano kuhusu dira ya taifa ya 2050 na uzinduzi wa Tuzo za Rais kwa Mzalishaji Bora Viwandani

SHIRIKISHO la Wenye Viwanda (CTI), limependekeza maendeleo ya viwanda yapewe kipaumbele kwenye Dira ya Taifa ya 2050.

Hayo yamesemwa leo jijini Dar es Salaam na Mwenyekiti wa CTI, Leodegar Tenga wakati wa mjadala wa wadau wa viwanda wakijadili Dira ya 2050 na kuzungumzia maendeleo ya viwanda kwa ujumla.

Mkutano huo ulioandaliwa na Shirikisho la Wenye Viwanda (CTI), pia ulizindua tuzo za Rais za Mzalishaji Bora Viwandani PMAYA ambazo hufanyika kila mwaka kwa wenye viwanda.

 Tenga alisema hakuna  nchi duniani hata moja ambayo iliwahi kupiga hatua kubwa kiuchumi bila kuwekeza kwenye viwanda kwa hiyo lazima kuwe na mikakati madhubutu ya kukuza viwanda.

 “Kuna msemo wa Kiswahili kwamba kupanga ni kuchagua kwa hiyo tuchague kuwekeza kwenye viwanda ili tusonge mbele na ili viwanda vifanyekazi vizuri lazima tuwe na watalamu wetu kwa hiyo tena lazima tuwekeze kwenye elimu bora,” alisema Tenga

 Alisema ili viwanda viweze kufanyakazi vizuri lazima serikali iwekeze pia kwenye ujenzi wa miundombinu ya barabara na reli na kuwekeza kwenye rasilimali watu.

“Maono ya nchi ni kujipanga ili tutimize tulichopanga kwa hiyo sisi CTI tunaamini viwanda ni muhimu na ili kupata rasilimali lazima tuwe na kilimo kwa hiyo lazima tuwekeze pia kwenye kilimo,” alisema

“Tumefungua masoko mengi upande wa Afrika Mashariki (EAC),  kusini mwa jangwa la sahara (SADC) sasa tujipange kuuza bidhaa zetu za viwandda nje ya nchi badala ya sisi kuwa soko la bidhaa za wenzetu,” alisema Tenga
 Naye Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Mipango na Uwekezaji), Prof Kitila Mkumbo alisema katika maandalizi ya Dira ya Taifa  2050 imeweka kipaumbele kikubwa kwenye maendeleo ya ya viwanda nia ikiwa ni  kuondoa utegemezi wa kununua bidhaa nyingi nje ya nchi.

Profesa Mkumbo alisema wasomi mbalimbali wamesema kwenye maandiko yao kuwa tofauti kubwa baina ya nchi tajiri na zile maskini ni kwamba nchi tajiri zina viwanda vingi wakati nchi maskini hazina viwanda na zinategemea kununua bidhaa nje ya nchi.

“Itakuwa vigumu sana kutengeneza Dira ya Taifa bila kuweka viwanda katikati ya dira hiyo kwasababu hilo ni la msingi na tafiti nyingi zinaonyesha kuwa hatuwezi kuendelea kwa kuendelea kununua bidhaa nje ya nchi, lazima tuwe na viwanda vingi tuuje  nje,” alisema

Alisema katika utafiti ambao umefanywa na serikali katika maandalizi ya dira hiyo uliohusisha watu 7,668 nchi nzima waliochaguliwa kisayansi walitaka vipaumbele vitano viwepo kwenye dira hiyo.
Alitaja moja ya kipaumbele kilichotajwa na wananchi hao kuwa ni suala la viwanda na kwamba asilimia 65 ya malighafi zinazotumika viwandani zinatokana na kilimo  hivyo kilimo nacho kitaendelea kuwa kipaumbele kwenye dira hiyo.

Alisema kipaumbele kingine kilichotajwa kwenye utafiti huo ni uwekezaji mkubwa kwenye rasilimali watu kwani uchumi wa viwanda unahitaji watu waliosoma vizuri.

“Lazima dira yetu ituelekeze kuwekeza kwenye elimu na siyo elimu tu bali elimu iliyobora,” alisema Profesa Mkumbo.