BoT yatangaza mabadiliko viwango vya riba vya Hati Fungani za Serikali

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 05:17 PM Dec 31 2024
Benki Kuu ya Tanzania (BoT).
Picha:Mtandao
Benki Kuu ya Tanzania (BoT).

Benki Kuu ya Tanzania (BoT), imetangaza mabadiliko makubwa yatakayotekelezwa katika utaratibu wa kuweka viwango vya riba kuanzia Januari 2025.

BoT ambayo ni wakala wa utekelezaji wa sera ya fedha ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, imewataarifu wawekezaji wa Hati Fungani za Serikali na umma kwa ujumla kuwa mabadiliko hayo yanalenga kuhakikisha viwango vya riba vya Hati Fungani za Serikali vinaendana moja kwa moja na hali halisi ya soko wakati wa mnada. 

Hatua hiyo inalenga kuimarisha masoko ya fedha nchini kwa kuongeza ukwasi, kurahisisha upatikanaji wa viwango sahihi vya riba, na kuongeza ufanisi wa soko la fedha.

Mabadiliko Yatakavyofanya Kazi

Hapo awali, viwango vya riba vya Hati Fungani za Serikali vilikuwa vikipangwa na kubaki bila kubadilika kwa kipindi kirefu, jambo lililochangia utofauti mkubwa kati ya viwango hivyo na riba halisi zinazopatikana katika masoko ya fedha. Kupitia utaratibu mpya:

  • Kiwango cha Riba Kutangazwa Kabla ya Mnada: Kiwango cha riba katika kila mnada wa Hati Fungani kitatangazwa angalau wiki moja kabla ya tarehe ya mnada. Taarifa hizi zitatolewa kupitia tovuti rasmi ya Benki Kuu, magazeti, na mitandao ya kijamii kupitia tangazo la zabuni la mnada husika.
  • Kuondolewa kwa Kiwango cha Riba kwenye Kalenda ya Minada: Tofauti na ilivyokuwa hapo awali, viwango vya riba havitatangazwa kwenye Kalenda ya Minada.
  • Utaratibu wa Ushiriki Kubaki Bila Mabadiliko: Wawekezaji wataendelea kushiriki katika minada ya Hati Fungani za Serikali kupitia mawakala walioidhinishwa, wakiwemo benki za biashara na madalali wa Soko la Hisa la Dar es Salaam.

Athari za Mabadiliko

Mabadiliko haya hayataathiri Hati Fungani za serikali zilizotolewa kabla ya Januari 2025. Hivyo, wawekezaji waliowekeza katika hati fungani hizo hawataona tofauti yoyote katika viwango vya riba walivyopangiwa awali.

Benki Kuu ya Tanzania itaendelea kuendesha minada ya Hati Fungani za Serikali kama ilivyoainishwa katika Kalenda ya Minada. Hatua hiyo ni sehemu ya juhudi za kuhakikisha kuwa masoko ya fedha yanakuwa imara na yanayotegemewa kwa maendeleo endelevu ya uchumi wa taifa.

Benki Kuu ya Tanzania (BoT).