BoT yakana kukiuka sheria matumizi Sh. trilioni 1.742/-

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 08:41 AM Jul 23 2024
Mkurugenzi wa Huduma za Benki BoT, Agaton Kipandula.
Picha: Mpigapicha Wetu
Mkurugenzi wa Huduma za Benki BoT, Agaton Kipandula.

UONGOZI wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) umetoa ufafanuzi kuhusu Sh. trilioni 1.742 zilizochukuliwa na serikali katika benki hiyo mwaka 2022/23, kwamba uko kisheria.

BoT imesema sheria iliyoiunda ya mwaka 2006 imeipa mamlaka ya kuipa serikali mkopo wa muda mfupi ili kuziba pengo au nakisi ya bajeti, hivyo hata kiasi tajwa hapo juu kilitolewa kwa msingi huo.

Imesema sheria hiyo inaisimamia BoT katika uendeshaji shughuli za serikali, ikiwamo kutoa huduma ya mikopo ya muda mfupi wa siku 180, lakini mkopo huo haupaswi kuzidi asilimia 18 ya mapato ya serikali kwa mwaka uliopita.

Mkurugenzi wa Huduma za Benki BoT, Agaton Kipandula, ndiye aliyetoa ufafanuzi huo jana jijini Dar es Salaam baada ya gazeti Nipashe Jumapili kuripoti kuhusu lilichokiita utata wa Sh. trilioni 1.7 kutolewa BoT.

Nipashe Jumapili iliripoti kuwa Sh. trilioni 1.742 zilizotolewa BoT katika mwaka 2022/23 na kutumiwa na serikali ilhali hazikuwa sehemu ya makusanyo ya serikali kwa mwaka huo wa fedha.

Akitolea ufafanuzi kuhusu fedha hizo, Kipandula alisema: "Benki Kuu ya Tanzania iko kwa mujibu wa sheria ya kuanzishwa kwake, Sura 197 na sheria tunayotumia sasa ni ya mwaka 2006.

"Kwa mujibu wa sheria hii, BoT ni benki ya serikali, hivyo fedha zote za serikali na mashirika au taasisi za umma zinatuzwa BoT."

Kipandula alisema sheria hiyo pia imetoa nafasi kwa BoT kutoa mkopo wa muda mfupi kwa serikali. Alisema mkopo huo kwa mujibu wa sheria unaitwa 'advance'; lengo lake ni kurekebisha kushuka na kupanda kwa mapato ya serikali.

"Kwahiyo, kupitia kipengele hicho, ndicho kinaifanya BoT ikopeshe serikali kwa muda mfupi. Sheria hiyo imeipa ukomo serikali wa kukopa ambayo ni asilimia 18 ya mapato yake.

"Mkopo huo ni wa ‘offset fluctuation’ (kuziba pengo/nakisi)). Kwa mfano, umekusanya Sh. 10,000 na unataka kulipa Sh. 15,000, ile Sh. 5,000 ndiyo inatengeneza mkopo. Na kadri siku zinavyokwenda kila mwisho wa mwezi serikali inarudi katika nafasi yake na kuwa sawa," alisema.

Kipandula alisema hata katika vitabu vya serikali, mkopo huo huwa hauonekani kwamba ilikopeshwa.

Alipoulizwa kama Bunge liliidhinisha serikali kupatiwa mkopo huo kama Sheria ya Bajeti inavyoelekeza, Kipandula alisema: "Bunge haliwezi kuidhinisha hili kwa sababu lengo si kutoa 'finance', serikali ina bajeti yake. Sheria ya Bajeti sisi BoT si sehemu ya mandate yetu, ipo chini ya Wizara ya Fedha."

Inaporejewa Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa Mwaka 2022/23 kuhusu suala hilo, inaonesha kuwa katika mwaka huo wa fedha, serikali ilikusanya Sh. trilioni 41.880 ikiwa ni zaidi ya bajeti ya Sh. trilioni 41.480 kwa Sh. bilioni 400.

CAG anafafanua kuwa kati ya Sh. trilioni 41.880 zilizokusanywa, Sh. trilioni 38.447 zilipokewa Mfuko Mkuu wa Hazina ya Serikali, hivyo kuwapo tofauti ya Sh. trilioni 3.4334.

CAG anasema tofauti hiyo inatokana na Sh. trilioni 3.656 zilizopelekwa moja kwa moja kwenye miradi kutoka kwa wadau wa maendeleo na makusanyo yaliyopelekwa Zanzibar ambayo hayapitii Mfuko Mkuu wa Hazina ya Serikali pamoja na Sh. bilioni 223 zinazotokana na bakaa za makusanyo ya kodi za mwaka uliopita na makusanyo mengine yaliyopokewa Mfuko Mkuu wa Hazina ya Serikali nje ya makisio ya bajeti.

"Jumla ya matumizi yaliyofanywa katika Mfuko Mkuu wa Hazina ya Serikali ili kugharamia matumizi ya kawaida na maendeleo kwa mwaka wa fedha 2022/23 yalikuwa Sh. trilioni 39.523 bila kujumuisha Sh. bilioni 665.80 zilizotolewa kama fedha zilizorejeshwa (refunds) na matumizi mengine kwenye jumla ya makusanyo ya Sh. trilioni 38.447, hivyo kusababisha nakisi katika Benki Kuu (BoT) ya Sh. trilioni 1.742 kufikia tarehe 30 Juni 2023," CAG anaeleza katika Ripoti yake ya Ukaguzi wa Hesabu za Serikali Kuu.