Watoto wanatamani elimu, wasaidiwe

By Sabato Kasika , Nipashe
Published at 12:41 PM Sep 24 2024
Waziri wa wizara hiyo, Dk. Dorothy Gwajima
Picha: Mtandao
Waziri wa wizara hiyo, Dk. Dorothy Gwajima

KATI ya Julai 2021 hadi Aprili mwaka huu, Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Wanawake, Jinsia na Makundi Maalum, imewaunganisha watoto 1,346 na familia zao.

Watoto hao ni miongoni mwa 6,459 ambao wizara hiyo iliwabaini wakati wa kutambua watoto wanaoishi na kufanya kazi mitaani, ambapo pia 816 kati ya hao wakiunganishwa na mafunzo ya stadi za maisha.
 
 Hayo ni kwa mujibu wa Waziri wa wizara hiyo, Dk. Dorothy Gwajima, akifafanua kuwa maeneo yenye watoto wengi ni Dar es Salaam, Mbeya, Arusha, Mwanza, Dodoma na Iringa.
 
 Pamoja na jitihada hizo, bado katika maeneo ya mijini, imekuwa ni jambo la kawaida kukuta watoto wenye umri wa kwenda shule, wakiomba msaada wa fedha na wengine wakiuza vitu vidogo kama karanga, pipi, biskuti na vitu vingine kadhaa.
 
 Zipo sababu mbalimbali zinazotajwa kuchangia uwapo wa watoto hao mitaa, ambao kama hakutakuwa na juhudi za makusudi za kuwanusuru, taifa linaweza kuwa watu wazima wa baadaye wasio na msaada.
 
 Miongoni mwa sababu hizo ni kutengana kwa wazazi wao au wote kufariki dunia, hivyo kuwalazimisha kutafuta maisha kwa kuomba msaada wa fedha au kufanya biashara ndogo ili kujipatia kipato.
 
 Inasikitisha kuona watoto wa umri wa kuwa shuleni, lakini badala yake wanakaa mitaani bila kupata elimu, ambayo huenda baadhi wangekuwa wataaalamu wa fani mbalimbali wa baadaye kama wangesoma.
 
 Ninadhani ni vyema kuwa kuwapo kwa hatua madhubuti za kukabiliana na mazingira hayo, ili kunusuru kizazi kijacho ili kiwe na faida kwa taifa lao, kwa kutambua kuwa vijana ni taifa la kesho.
 
 Mojawapo ya hatua ambazo zinapaswa kuchukuliwa, ni wazazi na walezi kuzingatia malezi bora na kuepuka mifarakano ili kuwafanya watoto  watulie nyumbani badala ya kukimbilia mitaani.
 
 Wadau wote wakiwamo wa ustawi wa jamii, waendelee kuelimisha umma umuhimu wa malezi bora, ili kusaidia watoto wenye umri kutulia nyumbani na kwenda shule, wasome badala ya kurandaranda mitaani wakiomba msaada au kufanya biashara ndogo, kwa sababu ya changamoto za wazazi wao.
 
 Lakini pia serikali ipige marufuku watoto na vijana wenye umri wa kwenda shule kurandaranda mitaani au kufanya biashara kwenye vituo vya mabasi. Kitendo ambacho kinachangia kuwafanya wakose elimu.
 
 Marufuku iwe ni ya kudumu na iende sambamba na mikakati ya kuwawezesha kupata elimu, badala ya kuwaondoa leo, lakini baada ya siku chache wanarudi tena mitaani kuendelea kuomba.
 
 Imekuwa ni jambo la kawaida kwa miaka mingi kuona wakiondolewa mitaani lakini baada ya siku chache huwa wanarudi. Kitendo ambacho kinaonyesha kuwa huenda hakuna hatua madhubuti.
 
 Si vibaya wakaondolewa na kupelekwa vituo maalum vyenye shule chini ya uangalizi, ili waweze kupata elimu, kwani katika kundi hilo, inawezekana wapo wenye vipaji lakini hawajapata fursa.
 
 Vilevile, jambo la msingi ni kuimarisha idara zinazohusiana na masuala ya elimu ya malezi, makuzi na maendeleo ya awali ya mtoto. kisha Wizara ya Maendeleo ya Jamii, ambayo moja ya majukumu yake ni kuratibu na kuitafutia majibu changamoto hiyo, ifanye kazi yake.
 
 Wanaweza kuwachukuliwa na kuwapeleka kwenye vituo vya serikali ya kulelea watoto wenye mahitaji maalum hasa wenye kuhitaji shule, kwani elimu ni muhimu kwa mtoto, hivyo, anapaswa kuipata.
 
 Ingawa kuwaita watoto wa mitaani kunapingwa kwa maelezo kuwa mitaa haizai watoto, ninakosa jina la kuwaita. Lakini hata liwe jina gani jambo la msingi ni kuwatoa katika mazingira hayo.