ELIMU ya awali kwa mtoto ni ya muhimu, kwani humjengea mtoto msingi mzuri wa kujua kusoma, kuandika na kuhesabu (KKK), humjenga na kumwandaa kujiunga na elimu ya msingi.
Mbali na hayo, elimu hiyo humsaidia mtoto kujua kumudu stadi za awali na pia humsaidia kujua stadi mbalimbali za ubunifu na kukuza lugha na kupanua uelewa wake kwa kujua vitu mbalimbali vinavyomzunguka.
Hatua hiyo ni muhimu ikilinganishwa na watoto ambao hawakupata elimu hiyo. Hivyo, wazazi na walezi hawana budi kuhakikisha wanawapeleka shule ili kupata elimu ya awali.
Serikali ilishaweka utaratibu kwa kila shule ya msingi kuwa na madarasa ya elimu ya awali, kwa ajili ya watoto wadogo ili wanapoanza elimu ya msingi wawe tayari wameshapata maarifa hayo.
Wakati huu tunapoelekea mwisho wa mwaka, wataandikishwa watoto wa elimu ya awali na darasa la kwanza, hivyo ni vyema asiwepo mzazi au mlezi mwenye visingizio vya aina yoyote ya kutomwandikisha mtoto.
Ni karibu miaka 10 sasa elimu inatolewa bure, hivyo hakuna sababu ya kuendelea kukaa na watoto nyumbani kwa kisingizio cha kukosa ada au kumficha mtoto kwa sababu ya ulemavu ama kwa namna yoyote ile.
Ikumbukwe kuwa, Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDG’s) hususani katika lengo Namba 4 la Elimu, ni muhimu jamii kusaidiana na serikali kusimamia na kutimiza lengo hilo kwa kishindo.
Lengo hilo linalofikia mwaka 2030, linagusa mambo mengi ikiwamo ubora wa elimu, ikiwa ni kujenga na kuboresha miundombinu ambayo itachangia mazingira bora ya kujifunza kwa watoto kwa wote.
Inaelezwa kuwa katika nchi maskini duniani, watoto na vijana wenye umri wa kwenda shule, hukabiliwa na changamoto kadhaa, ikiwamo watoto wa kike kutoenda shule, kwa sababu ya kulazimishwa kuolewa.
Vilevile, walemavu kunyimwa haki ya kwenda shule kwa sababu ya kukosekana miundombinu toshelevu kwa mahitaji yao na watoto wanaokwenda shule kukabiliwa na mazingira duni ya kusoma.
Bahati nzuri Tanzania imepiga hatua katika safari ya utimizaji wa Malengo ya Maendeleo Endelevu, hasa katika lengo hilo, katika upande wa usajili watoto shuleni, hivyo juhudi hizo zisikwamishwe.
Wazazi na walezi wawawezeshe watoto wao kupata elimu ya awali kwa kuwaondolea vikwazo ambavyo kwa namna moja ama nyingine vinaweza kusababisha wasipate elimu, hasa elimu bora.
Serikali ilishaimarisha na kujumuisha elimu ya awali kwenye mfumo rasmi wa elimu na kuagiza kila shule ya msingi kuwa na darasa la elimu ya awali, ili kumpa kila mtoto fursa ya kupata elimu hiyo.
Hivyo, wazazi na walezi ambao hawana uwezo wa kifedha kupeleka watoto wao shule binafsi, hawana budi kuwapeleka katika madarasa ya elimu ya awali ambayo yapo kila shule ya msingi ya serikali.
Kuwapo darasa la elimu ya awali kunasaidia watoto kuanza elimu ya msingi wakiwa tayari wanajua kusoma, kuandika na kuhesabu, kuliko kuwaacha walivyo na kujikuta wakiwa 'mbumbumbu'.
Mtoto kuhitimu darasa la saba bila kujua kusoma na kuandika, ni matokeo ya kutoanzishwa elimu ya awali ambayo ni msingi mzuri kwake wa kumfanya apate uelewa mapema kabla kuanza elimu ya msingi.
Wazazi na walezi wakumbuke kuwa, uhaba wa madarasa katika shule za serikali, unasababisha wanafunzi kurundikana katika chumba kimoja cha darasa na kusababisha ufundishaji na ujifunzaji kuwa mgumu.
Kwa mazingira kama hayo, si rahisi mwalimu kumfikia kila mwanafunzi ama wanafunzi wote kumwelewa, hivyo wale ambao watakuwa hawajapitia elimu ya awali wanaweza wasijue kusoma na kuandika hadi wanahitimu darasa la saba.
Katika elimu ya awali, mwalimu unapaswa kumwezesha mtoto kujenga umahiri husika kupitia shughuli zilizobainishwa, mbinu, zana stahiki za kufundishia na kujifunzia na kupima maendeleo ya mtoto hatua kwa hatua.
Hayo ni baadhi ya yaliyomo kwenye mwongozo Taasisi ya Elimu Tanzania (TET) ambayo imeandaa mtaala na muhtasari wa elimu ya awali unaolenga kuwajengea watoto umahiri uliokusudiwa.
Mwongozo huo umegawanyika katika sura nne, sura mbili za mwanzo zinatoa maelezo mafupi kuhusu uchambuzi wa mtaala na ujifunzaji na ufundishaji katika elimu ya awali.
Sura ya tatu inahusu upimaji maendeleo ya mtoto wa elimu ya awali, na nyingine sura inatoa maelezo kuhusu maandalizi ya ufundishaji na namna ya kuwezesha ujenzi wa umahiri ambao mtoto wa elimu ya awali anastahili kuujenga.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED