KINADHARIA na kimantiki, inapotamkwa kuwapo kundi fulani linajitambulisha, pia kuwa watetezi wa haki za binadamu, basi hutakiwa kuonekana ya kweli.
Ndani ya hilo, hutakiwa kuwapo ilani na matamko mbalimbali yanayohusu wakati husika wa kutetewa na kupewa kipaumbele matamko hayo, ili jamii na wahusika waone ni kweli wanatetewa.
Hivi karibuni kuna jumla ya asasi za kiraia zaidi ya 300 zimejitokeza kukabidhi Ilani yao ya Uchaguzi ya Mwaka 2024/29 kwa vyama vyote vya siasa iliyopendekezwa na ambazo zimeshirikiana kuandaa ilani hiyo.
Ni tukio la mwanzoni mwezi huu, ambako Mratibu Kitaifa Mtandao Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC) Onesmo Olengurumwa, mbele ya vyombo vya habari walikabidhi ilani hiyo kwa vyama mbalimbali vya siasa vitakavyoshiriki uchaguzi wa serikali za mitaa na ule mkuu mwaka ujao.
Katika ilani hiyo, wamegusa maeneo mengi zikiwamo usawa wa kijinsia na katika tamko lao, wakasema serikali inahitaji viongozi watakaoimarisha uwakilishi wake katika nafasi zote za uongozi na uamuzi kwa kufikia lengo la ‘50 kwa 50’.
Lengo la usawa huo ni kuwataka viongozi hao wataboresha mazingira ya elimu kwa watoto hasa wasichana, ili kuongeza idadi ya wanawake katika masomo yanayoitwa ‘STEM’ na kuhakikisha elimu bora kwa wote.
Mapendekezo hayo pia yaligusa kufanya mapitio na marekebisho ya sheria kandamizi kwa wanawake, kama vile Sheria ya Ndoa ya Mwaka 1971; Sheria ya Mirathi ya Mwaka 1965 na Sheria za Kimila Na.4 ya Mwaka 1963, zote zikiwa na malengo ya kuondoa ukandamizaji na kuondoa ubaguzi dhidi ya wanawake na wasichana.
Walitaka viongozi wadhibiti mifumo inayowapa wenye mali madaraka makubwa ya kisiasa, kuimarisha demokrasia shirikishi na kuongeza ushiriki wa wanawake na wanaume maskini katika maamuzi ya kitaifa.
Aidha, walitaka viongozi kupiga marufuku matumizi ya lugha za kashfa, matusi na udhalilishaji kwenye chaguzi ili kuhakikisha ushiriki wa makundi yote bila ya vikwazo.
Vilevile mtazamo huo ukagusa kuongeza kasi ya kupambana na ukatili wa kijinsia katika jamii, ikiwamo rushwa ya ngono dhidi ya wanawake.
Katika Ilani, watetezi hao walitoa kinachoitwa ‘Tamko Dhidi ya Watoto’ na kutaka itungwe sheria inayoandaa miongozo ya kuwalinda watoto dhidi ya utandawazi usiokuwa na maadili.
Hapo yamo ya elimu inayotafsiriwa kwa ‘Elimu ya Magharibi’ yenye baadhi ya masuala yaliyo kinyume na mila na desturi za Mtanzania.
Mantiki ya hoja hiyo ni kuitaka serikali ije na mkakati madhubuti wa kuondoa watoto wa mtaani wenye umri wa kwenda shule na kutenga bajeti mahsusi ya kutekeleza mkakati wa kutokomeza tatizo hilo katika miji na majiji.
Dai lingine linaloangukia eneo hilo, linagusa haja ya kuwa na mkakati wa ulinzi na malezi jumuishi kwa mtoto wa kiume, katika kumwepusha na vitendo viovu, hasa ukatili wa kijinsia ili kumkuza katika mkondo wa maadili.
Wadau hao, wanataka mtazamo wa kuanza kutolewa elimu ya haki za binadamu kuanzia ngazi ya shule za awali, zikilenga kumjenga mtoto kuhusu haki za binadamu na haki zake katika nafasi yake ya utoto, aweze kukabiliana na njia bora za kudhibiti ukiukwaji haki za mtoto.
Serikali katika mustakabali huo, inatakiwa kupeleka huduma ya ustawi wa jamii kwa kata zote nchini, wahusika wanaoendesha wakipewa stadi za ziada kupitia mafunzo ya kila mara, kuhusu sheria na haki za mtoto na namna bora ya kutatua migogoro ya ndoa.
USALAMA WA WAZEE
Tamko lingine likawa katika ‘Ulinzi, Usalama na Ustawi wa Wazee’ wakivitaka vyama vya kisiasa katika michakato ya uchaguzi inayokuja, kuhakikisha kunakuwapo usalama wazee, wanaoshiriki shughuli za kisiasa, wasibughudhiwe, kuumizwa, kudhalilishwa na kufanyiwa ukatili wa aina yoyote.
Rai yao kwa serikali ni kuhakikisha inapata takwimu sahihi kuhusu wazee na kuwaunganisha na mifumo ya hifadhi ya jamii pamoja na fursa nyinginezo, wakitaka kuanzishwe utaratibu wa kuielimisha na kuijengea uelewa jamii katika eneo hilo.
Eneo la mtazamo unaelekezwa pia, katika yanayohusu kutunza na kulinda haki za wazee katika ngazi ya familia, ili kupunguza kasi ya kujengwa kwa makazi ya wazee.
Wanasiasa wanatakiwa kuwezesha kuwapo wafanyakazi wa afya, wapatiwe mafunzo maalum ya kutunza, kuwapokea na kuwahudumia wazee na hasa umuhimu wakuupa kipaumbele utunzaji wa afya kwa wazee.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED