KUNA kundi la vijana katika jamii, ambalo ni muhimu katika ujenzi wa taifa, kwa kuwa lina nafasi ya kutegemewa, kwani ni nguvukazi sahihi katika ustawi wa taifa.
Kundi hilo ni pana, linategemewa na katika kila nyanja, likitazamwa kuanzia ngazi ya familia, serikali, mashirika, taasisi zikiwamo asasi za kiraia katika kulijengea uwezo.
Hiyo ni kwa kuwa ndio nguvu kazi inayoleta tija kuliko makundi yote, mtazamo hapo linatakiwa kuwa kundi linaloangaliwa zaidi, kwani ndio ustawi wa jamii kwa ujumla.
Asasi za kiraia kwa jina lake maarufu azaki za kiraia, jumla yake 300 wakati zimeumiza vichwa kwa pamoja na kwa kulitakafari kundi hilo na kuliwekea mikakati.
Hapo kuna mapendekezo kadhaa ajenda yao ya Uchaguzi wa Serikali ya Mitaa Mwaka 2024 hadi 2029, waliyoikabidhi Oktoba mwaka huu kwa vyama vya siasa.
Ndani yake wamelitazama kwa kina kundi hilo, ili kuhakikisha ilani hiyo inalipigania kundi hilo lipate kuangaliwa zaidi, kutokana na umuhimu wake.
Azaki za kiraia zinazotetea haki za binadamu zilitoa tamko kuhusu kundi hilo la vijana wakitaka kuwapo uanzishwaji wa fursa za ajira na kuiwekea mifumo rafiki ya mchakato wa uombaji na upatikanaji ajira hizo, ndani ya sekta za umma na binafsi.
Hapa tujiulize, je kwa kundi hili kuna mifumo rafiki iliyowekwa katika uombaji na upatikanaji wa ajira katika sekta hizo kwa vijana wa mijini na vijijini?
Kama Magali hapo kuna ukweli, tupige hatua nyingine ya kuhoji namna mifumo hiyo iko rafiki kwa kundi hilo. Naipa kongole serikali, kutokana na uanzishwaji huo unaowawezesha vijana wapate ajira.
Lakini hapo hapo, kama mazingira hayo hayapo, basi kwa juhudi hizi naamini mifumo hiyo ya fursa za ajira iwe na usawa kati ya vijana wa mijini na vijijini na iwe na usawa kati ya waliokuwa nacho na wasiokuwa nacho, ili fursa hizo ziwafikie vijana wote.
Tunaona pia azaki hizo zimetaka kuboreshwa kwa mfumo wa elimu kwa vijana, wanapataje elimu na mafunzo kwa vitendo yanayowapa ujuzi na maarifa ya kuwawezesha kuwa wabunifu na zaidi kuwawezesha kujiajiri.
Kwa upande wangu, pendekezo hilo liko sawa na kwani elimu ikiboreshwa vyema kwa upande wa vijana itakuwa ‘bomba’, itapendeza! Kwani nadharia ‘vijana ni taifa la leo’ imegeuka, si ‘la kesho’ tena kutokana na zama tulizoko.
Aidha ilani ya wadau wanaharataki imedai kuanzishwe utaratibu wa kuwapa nafasi vijana kushiriki kwenye michezo inayokuza na kuendeleza vipaji vyao, kuanzia ngazi za shule hadi vyuoni, warahisishe vipaji vyao na taaluma.
Vilevile tumeona azaki hizo kwa pamoja, zinaitaka serikali itekeleze programu za uwezeshaji vijana usio na ubaguzi kwa misingi ya kiitikadi.
Hapo ni kuwapa fursa wote kushiriki katika shughuli za uzalishaji na kujipatia kipato.
Pia, napo naunga mkono hoja kama juhudi hizi walizopendekeza asasi hizo, basi tutakuwa na taifa lenye tija, kwa kuwa programu hizo zikianzishwa vijana ambao ndio taifa la kesho wataweza kujitengenezea vipato visivyo na mwisho.
Walitaka uandaliwe mfumo wa kuwezesha vijana wote kushirikiana katika shughuli za uchumi na kupata ujira stahiki bila kunyongwa.
Viongozi waanzishe utaratibu wa kuwatambua vijana wenye vipaji na ubunifu katika maeneo tofauti na kuviendeleza waweze kuongeza thamani ya vipaji hivyo viwaingizie kipato.
Ilani imelitazama hilo kwa kina kundi hili la vijana na kulitetea vyema, ili kulitaka liwe na ustawi kwa kuwa ndio taifa la leo na la kesho naunga mkono hoja.
Ilipendekezwa na kutengenezwa na zaidi ya asasi za kiraia 300 na iliwakilishwa ndani vya vyama vya siasa na Mratibu Kitaifa wa Mtandao wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC) Onesmo Olengurumwa.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED