MVUA ni mtaji mkubwa kwa mazingira, ingawaje zinapozidi nazo zinahamia upande wa athari katika maisha ya mazingira kijamii.
Hadi sasa mvua zinazonyesha kiasi katika maeneo mbalimbali ya mkoa wa Dar es Salaam, zimekuwa zikigusa moja kwa moja mustakabali wa biashara na wafanyabiashara katika masoko, ambayo miundombinu yake haipo vizuri.
Katika soko la Mabibo, Dar es Salaam ambako huingiza bidhaa kutoka mikoa mingine mbalimbali nchini na wanaofanya baadhi ya aina ya uchuuzi, wanakimbilia huko kupata bidhaa, mvua zinaponyesha sokoni humo, baadhi ya maeneo huwa na matope mengi sana.
Matope hayo katika soko hilo, yanawaibua kinamama nao wanatumia fursa hiyo kukodisha mabuti kwa watu wahitaji, kwa ya shilingi 1000.
Zuwena Juma, mkazi wa Mabibo, Dar es Salaam, anasema kuwa mvua zinaponyesha kwao hali hiyo ni neema, kwani ndio mwanzo wa kukodisha mabuti kwa watu wanaotaka kuingia sokoni.
"Mtu anatoa shilingi 1000, anaacha viatu vyake na akimaliza mizunguko yake anarudisha buti na kupewa viatu vyake," anasema.
Johari Shaban, anasema kwa kipindi cha mvua, buti jozi moja inauzwa shilingi 12,000, lakini kwa kipindi cha jua kali, jozi ya buti inauzwa shilingi 8000.
Anasema katika biashara hapakosi changamoto, wapo baadhi ya wateja wanaoacha viatu vyao na kuondoka na buti zao.
Pia, anafafanua kuwapo baadhi ya vijana wanauouza mifuko na wanaongozana na wateja waliochukuwa buti na wakizunguka nao hurudi, hata wanarudisha mabuti na kuchukuwa viatu vyao.
Zuwena anasema katika kufanya biashara hiyo ya kukodisha viatu, wanazingatia masuala ya afya na kanuni zake, akitumia mifano mteja anapovaa buti, hupewa mfuko wa plastiki ambao aivae kwanza na kisha ndio anavaa buti.
Mhusika mwingine, Aisha Jamali, anasema katika kipindi cha mvua, huwa anajiongezea kipato pale watu wanapokuwa na matope miguuni, huwa anawaosha miguu na anapatiwa shilingi 200.
"Kimvua kikinyesha kidogo, soko linakuwa na matope, wateja wengine hawana uwezo wa kukodi buti, hivyo wanayakanyaga matope na kuja kwangu kuoshwa miguu kwa shilingi 200," anasema, akiongeza kuwa mvua ikinyesha kwao ni neema kutokana na kujiingizia kipato.
Hadi sasa, Soko la Mabibo ambalo liko ndani ya Manispaa ya Kinondoni, Dar es Salaam, limekuwa na mijadala mingi kutoka kwa umma, mojawapo ikiwa ni kuhusiana na hali ya mazingira yake yalivyo kirafiki.
Hata hivyo inavyojulikana, kasoro moja inafaa upande wa pili wa shilingi, kwani magumu yanayopatikana ndio inafungua nafasi ya ahueni ya kiuchumi kwa jamii mahali hapo wanatafuta kipato.
Inaelezwa kwamba, kumekuwapo ugumu katika uendelezaji soko hilo kutoka upande wa manispaa, kwa mamlaka husika haina milki rasmi ya eneo hilo, hivyo inashindwa kuendeleza na ndio moja ya sababu soko hilo linabaki katika hali hiyo inayosimuliwa miaka yote.
Mbali na hilo, Soko la Mabibo, Dar es Salaam limebaki kuwa na hadhi yake ya kuwa kituo kikuu cha kushusha ndizi ndani ya Dar es Salaam, kutoka mikoa tofauti inakozalishwa.
Kwa ujumla, bado kuna tafsiri masoko mengi ambayo ni kama wakala ndani ya Dar es Salaam, katika kushusha bidhaa na hasa vyakula, kama vile Temeke Stereo, Ilala, Soko Kuu la Kariakoo na Tandale.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED