Miaka mitatu ya Samia imerudisha siasa za ushindani

By Sabato Kasika , Nipashe
Published at 03:59 PM Mar 24 2024
Rais Samia Suluhu Hassan.
PICHA: IKULU
Rais Samia Suluhu Hassan.

LEO ni siku ya sita tangu Rais Samia Suluhu Hassan atimize miaka mitatu madarakani, na sasa ameanza safari ya mwaka mwingine wa nne kuelekea uchaguzi wa serikali za mitaa na uchaguzi mkuu wa 2025.

Rais alikula kiapo kuongoza nchi Machi 19 mwaka 2021. Kabla ya hapo kulikuwa na malalamiko kutoka kwa vyama vya upinzani vikitamani kuwapo kwa uhuru wa vyama vya upinzani kufanya siasa za ushindani.

Malalamiko hayo yalitokana na zuio la mikutano ya hadhara ya vyama hivyo, lililowekwa na mtangulizi wake, hayati Dk. John Magufuli aliyeagiza madiwani na wabunge kufanya mikutano maeneo yao.

Zuio lingine lilikuwa ni la maandamano ya vyama kwamba viache serikali ifanye kazi, hatua ambayo ilisababisha malalamiko kutoka kwa wanasiasa na wadau wa siasa wakitaka vyama viwe huru kufanya siasa.

Katika kipindi cha miaka mitatu ambayo Rais Samia ameingia madarakani, amefanya mengi ya maendeleo, lakini bila kusahau siasa, kwa kuondoa zuio la mikutano na maandamano.

Rais amekuja kuboresha zaidi kile kilichowekwa na mtangulizi wake kwa kuweka wigo mpana wa kufanya siasa kwa kuruhusu mikutano ya hadhara ya vyama vya siasa ambayo awali ilizuiwa.

Amefanya hivyo, kwa kuzingatia mazingira ya sasa kulingana na katiba na sheria kuwa haki kwa sheria za nchi vyama kufanya mikutano ya hadhara, hivyo hakuona sababu ya kuwapo kwa zuio hilo.

Matamanio yake ni kutaka wanasiasa wapambane kwa usawa kama njia ya kuimarisha demokrasia ili kuwaleta Watanzania pamoja ili wapinzani wakiwa na hoja zenye mashiko, anazichukua kuzifanyia kazi.

Kimsingi uhai wa vyama vya siasa ni pamoja na mikutano ya hadhara, ambayo ni jukwaa muhimu linalosaidia wanasiasa kutangaza sera za vyama vyao kwa wananchi ili waviunge mkono.

Hivyo, kwa mazingira hayo na umuhimu wake, ndio sababu Rais Samia akaondoa zuio hilo, ili kutoa uwanja sawa wa siasa kati ya CCM na vyama vya upinzani, lakini pia apate hoja zao na kuzifanyia kazi.

Maana yake ni kwamba, ameamua kutowafunga midomo ili wajimwage watoe ya moyoni badala ya kuendelea kulalamikia kutokuwapo kwa uwanja sawa kati yaa vyama hivyo na CCM.

Kupitia uamuzi huo wa Rais wa kuzingatia sheria na katiba ya nchi, hata CCM nayo inakuwa na nafasi ya kujirekebisha kama hoja za upinzani zitakuwa zinaigusa na hivyo kuendelea kuaminika mbele ya umma.

Ninaamini kuwa hiyo ni karata nzuri ambayo Rais ameicheza ya kupanua wigo na kurudisha upinzani wa kisiasa ili anufaike zaidi kwa hoja za wapinzani wasiwe na lingine la kupeleka kwa wananchi.

Uamuzi huo wa Rais Samia, unaonyesha kuwa anawachukulia wapinzani kama kioo chake cha kufanya marekebisho pale wanapotoa hoja zao ili yeye na serikali wazichukue na kuzifanyia kazi.

Lakini pamoja na hayo, ninadhani vyama vya upinzani, vingetumia nafasi hiyo vizuri hiyo kwa kutangaza sera za vyama vyao badala ya kashfa au matusi dhidi ya viongozi wa serikali.

Ikumbukwe kwamba, Rais amekuwa mtu ambaye anapenda kukosolewa, hasa kwa kutambua kuwa yeye si malaika, lakini pia ni vyema ukosoaji huo ukawa wa lugha ya kistaarabu.

Kwa kuwa ameruhusu kukosolewa, suala la kuzingatia mila na desturi za kitanzania katika ukosoaji ni la muhimu, hasa kwa kuzingatia kwamba hatua hiyo inasaidia kudumisha umoja wa kitaifa.